Viroba vyapoteza bil. 600/- za serikali



SERIKALI imetangaza kutunga kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali ambazo zitaweka masharti ya kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashwe kwenye chupa zinazoweza kujazwa tena kwa ujazo usiopungua miligramu 250. Imesema, inapoteza Sh bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi kwenye biashara ya pombe hiyo.

Upigaji marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) unatokana na kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa Februari 16, mwaka huu mkoani Manyara ya kutaka kusitishwa utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio hivyo ifikapo Machi Mosi mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema kutokana na tamko hilo la Waziri Mkuu na tamko la serikali kuhusu dhamira hiyo lililotolewa bungeni Mei, 2, 2016, ofisi yake imeamua kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa maamuzi hayo ya serikali.

“Waziri mwenye dhamana ya Mazingira atatunga kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali kwa mujibu wa Kifungu 230(2)(f) cha Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004,” alisema January na kuongeza kuwa kanuni hizo pia zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji nchini na matumizi ya pombe zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya malighafi ya vifungashio vya viroba vitakavyotumika kufungashia pombe kali.

Alisema atakayebainika kukiuka masharti ya kanuni hizo, atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja kama itakavyoainishwa kwenye kanuni.

“Dhamira ya serikali siyo kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali, bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya. Haki hiyo pia imetiliwa mkazo katika Sheria ya Mazingira ya 2004,” alifafanua waziri huyo.

Alisema dhamira ya serikali ni kudhibiti upatikanaji wa pombe kali kwa urahisi kunakotokana na kufungwa katika plastiki na kwa ujazo mdogo, kunakopelekea kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali hadi kwa watoto wadogo, kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuzagaa kwa vifungashio hivyo.

Pia alisema wamelenga kudhibiti ukwepaji mkubwa wa kodi kutokana na urahisi wa teknolojia na gharama za kutengeneza pombe kali inayofungashwa kwenye viroba rasmi ambapo inakadiriwa kwamba serikali inapoteza Sh bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi kwenye biashara ya pombe za viroba.

“Utekelezaji wa manunuzi haya ya serikali unaanza mara moja. Ingawa haitegemewi, lakini iwapo kuna wazalishaji watakaohitaji muda wa ziada wa kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, wataomba kibali maalumu cha muda mfupi ambacho hakitatolewa hadi muombaji awasilishe nyaraka maalum zitakazohitajika kabla ya Februari 28,” alibainisha waziri huyo.

Alisema zipo pombe za viroba zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi hasa kwenye mikoa na miji ya mipakani, hivyo wakuu wa wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Kamati za Mazingira, wanaelekezwa kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia viroba vinavyoingizwa kinyume cha utaratibu na pia itahusu uporesheni ya pombe haramu ya gongo.

Aidha, alisema serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa hatua hizo na kinajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Wengine ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Chakula na Dawa, Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi.

Alisema doria za ukaguzi wa utekelezaji wa hatua hizo zitaanza wakati wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka ambapo Ofisi ya Makamu wa Raisi itaratibu kikosi hicho.

Kuhusu mifuko ya plastiki, alisema kanuni za udhibiti zinaandaliwa na zuio litatangazwa wakati wowote na kuwataka wazalishaji, waingizaji na wauzaji wa mifuko hiyo nao kujiandaa.

Alisema hatua hizo za serikali siyo za ghafla au kushtukiza kwani taarifa ilishatolewa bungeni takribani mwaka mmoja sasa na pia serikali ilitoa taarifa rasmi Agosti mwaka jana na Desemba kuhusu dhamira ya kuchukua hatua hizo, hivyo wanaamini wazalishaji wa pombe za viroba na mifuko ya plastiki watakuwa wamejiandaa kubadilisha teknolojia.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment