WASOMI, wanasiasa wakongwe, wachambuzi wa kisiasa na viongozi wa dini nchini, wamepongeza muundo mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofikiwa juzi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais John Magufuli.
Wameeleza kuwa muundo huo, utakiwezesha chama kushindana vizuri kisiasa.
Aidha wamesema Magufuli anavaa viatu vya Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika muundo huo wa idadi ndogo ya watendaji makini, lakini pia utasaidia kulinda siri za chama, kubana matumizi na kuwajibika ipasavyo kuisimamia Serikali.
Wamepongeza hatua ya Mwenyekiti wa chama hicho, Magufuli, ambaye pia ni Rais wa Tanzania, kumbakiza Katibu Mkuu wa chama, Abdulrahman Kinana kwani imeonesha kuthamini kazi kubwa aliyofanya katibu mkuu huyo ya kufufua chama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kuwa maamuzi hayo yamefanyika kwa wakati muafaka na yalikuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya alisema uamuzi uliofanywa na Magufuli walikuwa wakiyasubiri kwa muda mrefu, kwani ndiyo muundo uliokuwepo siku za nyuma chini ya uenyekiti wa Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mzindakaya ambaye ni mwanachama wa chama hicho, alisema chama kikubwa kama hicho mabadiliko ni muhimu, kwa lengo la kujenga hali mpya kwa wanachama wake kwa ajili ya maslahi ya chama na wanachama wake.
Alisema kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu, walikuwa wengi zaidi ya wabunge, lakini awali kila mkoa ulikuwa na mjumbe mmoja, lakini kwa sasa kila wilaya kulikuwa na mjumbe, jambo lililofanya kudhoofisha nguvu ya chama na kutoka kwa siri za chama nje mara baada ya kikao.
“Kawaida maamuzi makubwa ya chama yanayofanyika ni siri, lakini hali ilikuwa tofauti kwani kila siri ilikuwa ikitoka nje; huku kuwa na utitiri wa viongozi kulisababisha chama kupata gharama kwa kuwalipa pale inapoitishwa mikutano ya Halmashauri Kuu,”alisema.
Dk Mzindakaya ambaye alikuwa waziri katika serikali zilizopita, alisema katika uteuzi wa wataalamu kwenye sekretarieti ni muundo muhimu, kwani sekretarieti ipo kwa ajili ya kumsaidia katibu mkuu.
Alisema kazi za kiutendaji hazitakiwi kufanywa kwa siasa, bali kwa kutumia utaalamu hivyo Mwenyekiti amefanya jambo sahihi.
Alisema pia ndani ya chama hicho, kulikuwa na tabia ya baadhi ya watu kujilimbikizia vyeo, kwani ilikuwa si jambo la ajabu kumuona mbunge akiwa pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wakati mwingine ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa.
Alisema jambo hilo lilisababisha wanachama wengine kukosa fursa kutokana na wajumbe hao, kulinda maslahi yao binafsi ya kisiasa na kiuchumi.
“Uamuzi huu kwa kweli wa kubadili muundo ni muhimu sana na unapaswa kupongezwa kwani kuna watu walikuwa na vyeo vingi katika chama kwa maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi huku wakiwakosesha wanachama wengine wenye uwezo fursa ya kukiendesha chama,“ alisisitiza Dk Mzindakaya.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Dk Benson Bana alimpongeza Mwenyekiti wa Chama hicho kwa hatua aliyoifanya, kwani ameonesha kuwa anataka kuwa na CCM mpya.
Alisema mabadiliko anayoyapendekeza, yanayohusu marekebisho ya katiba, ni marekebisho chanya kwa uhai wa chama na kukipa chama nguvu mpya ya kukabiliana na mazingira ya kisiasa ya leo na chama kukirudisha kwa wananchama.
“Hiki ni chama cha wanachama kwaajili ya wanachama na alichokifanya Magufuli ni kuonesha nia ya kufanya,” alisema Bana.
Pia, alisema jambo alilolifanya Magufuli, la kupunguza mlolongo wa matumizi na vikao na wajumbe ndani ya vikao, ni jema na litasaidia mno chama.
“Hatuna ushahidi kama wingi wa wajumbe wengi, ndio ubora wa vikao, unaweza ukawa na wajumbe wachache na ukafanya jambo zuri; na siku zote mambo mazuri hayafanywi na watu wengi, yanafanywa na watu wachache na Magufuli ameliona hilo,” alisema Bana.
Aidha, alisema suala la kufuta vyeo mbalimbali katika chama, ni jambo zuri kwakuwa limeondoa wale watu ambao walitaka kukishikilia chama na kuona wa ndio wenye chama.
“Wapo waliokuwa ni makamanda wa chama, mara kamanda wa vijana, au mlezi wa wazazi. Haya yote yalikuwa yanazidisha chuki, fitina na ushindani usio na tija ndani ya chama, kwahiyo ni vizuri ameyafuta haya,”alisema.
Pia, alimpongeza Rais kwa kuwateuwa vijana ambayo ni damu mpya na kuwaacha wazee.
“Tunaamini vijana walioteuliwa, wanaweza kuhimili mikikimikiki kujibizana na vijana wa vyama vigine. Kwenye sekretarieti tungependa kati ya watatu aliowachagua mmoja angekuwa mwanamke, lakini nadhani kwa sasa hivi nguvu zake zipo kwenye kuleta ufanisi zaidi kuliko mambo mengine,”aliongeza.
Mwanasiasa maarufu Profesa Mwesiga Baregu alisema mabadiliko aliyofanya Magufuli lazima yatakuwa na sababu zake; na kwamba labda mwenyekiti huyo wa chama, ameona hawezi kufanya kazi na watu wengi.
Alisema kwa upande mwingine, mabadiliko hayo yanaweza kubinya demokrasia, lakini pia ameangalia watu wa kufanya kazi naye.
Baregu alisema kiini cha mabadiliko hayo, hakijajulikana, lakini amefumua muundo wa chama hicho kwa kuwatoa wale waliokuwemo katika uongozi wa awamu ya nne.
Wakati huo huo, Askofu wa Kanisa la Good News for All Ministry, Dk. Charles Gadi amekipongeza chama hicho cha CCM kwa mabadiliko waliyoyafanya na kuingiza vijana katika safu ya uongozi.aa
Askofu Gadi alisema chama hicho kimeonesha ukomavu wa kisiasa, hasa kwa kukiamini kizazi cha vijana ambao wanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuutendaji ndani ya chama hicho.
“Tunaamini kwamba CCM kwa kuwaweka vijana wengi watafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu vijana hawa tayari walishaonesha utendaji wao katika maeneo tofauti,” alisema.
Aidha alisema hatua ya CCM kupunguza idadi ya wajumbe, itapunguza gharama za uendeshaji, hivyo kuongeza ujenzi wa miradi mbalimbali kupitia fedha hizo.
“Tunaamini kwamba kwa kupunguza gharama ya wajumbe, fedha hizo zinaweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo kujenga shule, maabara, madawati, hospitali na kuongeza upatikanaji wa dawa hospitalini,” alisema.
Katika kikao hicho cha NEC kilichofuatia kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kilichokaa Jumapili, idadi ya wajumbe wa NEC ilipunguzwa kutoa wajumbe 388 hadi wajumbe 158, ikiwa na maana kuwa wajumbe 200 wataondolewa kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kutoka 34 hadi 24, wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa wamepunguzwa watatu, wakati wilayani wameondolewa wanne; pamoja na kufutwa kwa vyeo vya Makatibu Wasaidizi wa Wilaya na Mikoa na wa Mchumi wa Wilaya na Mkoa.
Pia nafasi za uteuzi za wajumbe wa NEC za Mwenyekiti, zimepunguzwa kutoka 10 hadi saba.
Magufuli alisema hatua hiyo ni ili kutoa nafasi kwa viongozi na wanachama, kufanya kazi za chama kwa ufanisi Aidha, Magufuli alimbakiza katika nafasi yake ya Ukatibu Mkuu, Kinana huku sura mpya katika jamii zikichukua nafasi kubwa za uongozi katika chama hicho.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Rodrick Mpogolo aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu upande wa Tanzania Bara na Humphrey Polepole anayekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, akichukua nafasi ya Nape Nnauye ambaye ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Yumo pia Kanali Ngemela Lubinga aliyeteuliwa kuwa Katibu wa NEC wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mbali na uteuzi, pia Magufuli alisema kwa kuwa kumekuwa na vitu na watu hewa katika kila eneo nchini, pia katika CCM kunahitajika uhakiki wa wanachama hewa.
Katika uhakiki huo utakaofanyika nchi nzima, pia alisema chama kitaanzisha mfumo wa kadi za kieletroniki na kuachana na kadi za sasa, zikiwamo za jumuiya yake ambazo zinafutwa rasmi.
Mabadiliko hayo makubwa ambayo baadhi yanahusisha Kanuni na Miongozo, yataanza mara moja na yale yanayohusisha Katiba ya CCM, yatapata idhini ya Mkutano Mkuu utakaoitishwa Februari mwakani na yamehusisha pia kufutwa kwa baadhi ya nyadhifa.
Aliposhika hatamu za CCM mjini Dodoma, katika hotuba yake, Dk Magufuli alieleza azma yake ya kuijenga CCM mpya, ikiwamo kuondokana na vyeo visivyokuwa na tija na pia kupunguza idadi ya wajumbe wakiwamo wa NEC
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
0 Maoni:
Post a Comment