MSHITAKIWA
katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Salum Njwete (34)
‘Scorpion’, amekiri kupata mafunzo ya kareti kutoka chuo cha mafunzo cha
Ifakara aliyoyafanya mwaka 1989 hadi 1995.
Aidha,
upande wa mashitaka katika kesi hiyo umemuongezea mashitaka ya
shambulio kupitia kifungu namba 234 cha Sheria ya Makosa ya Jinai
ambacho kinaruhusu kuongeza au kubadilisha mashitaka.
Wakili
wa Serikali, Nassoro Katuga alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Flora
Haule kwamba kesi hiyo imekuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo
ya awali ambapo katika maelezo ya zaidi ya saa nane, alikiri kuhusu jina
lake, sehemu anayoishi ya Machimbo Yombo na mafunzo hayo.
Hata hivyo, alikana kuhusu jina la Scorpion, mashitaka yake na kwamba hakukamatwa wala kuhojiwa na Polisi kuhusu mashitaka hayo.
Katuga
alidai kuwa Septemba 6, mwaka huu, mshitakiwa alikuwa maeneo ya
Buguruni Sheli na kwamba Septemba 12, alihojiwa na kukamatwa na polisi
maelezo ambayo aliyakana.
“Mashahidi
watakaotoa ushahidi katika kesi hii wapo sita ambapo upande wetu wa
mashitaka utawasilisha vielelezo viwili ikiwemo Fomu namba tatu ya
Polisi (PF3) na ripoti ya daktari kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka
hayo,’’ alidai Katuga.
Hakimu
Haule aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 14 mwaka huu, kesi hiyo
itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa. Katika mashitaka yake, mtuhumiwa
inadaiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu katika maeneo ya
Buguruni Sheli, wilaya ya Ilala.
Inadaiwa,
Njwete aliiba mkufu rangi ya fedha wenye uzito wa gramu 34 wenye
thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi na fedha taslimu Sh 331,000,
vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Said Mrisho.
Inadaiwa kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie mali hizo.
0 Maoni:
Post a Comment