Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa habari uliofanyika jana Dar es Saalam na kuandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nape alisema ni vyema wanahabari wakabainisha maeneo yenye upungufu kwenye sheria hiyo ili yafanyiwe kazi.
“Sheria imekuja wakati ambao dunia ipo kwenye mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, waandishi wa habari wanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko hayo na huo ndiyo msingi mkubwa wa sheria hii hakuja haja ya kuiogopa au kuikataa,maeneo yenye upungufu yabainisheni ili yafanyiwe kazi,” alieleza Nape.
Akifafanua, alisema sheria hiyo imezingatia maoni ya wadau wengi na kuna mambo waliyaona badala ya kuyaweka kwenye sheria ni vyema yakaingizwa kwenye kanuni ili iwe rahisi kuyafanyia marekebosho ikiwemo sifa ya mwandishi wa habari.
Aidha, alisema maoni ya wadau mbalimbali waliyotoa kuhusu sheria hiyo yatazingatiwa katika utungaji wa kanuni hizo ambapo ametaka wadau hao na wengine ambao hawajatoa kupeleka maoni yao haraka ili kuwezesha kanuni kutungwa na kutoa mwaya wa sheria hiyo kuanza kufanya kazi.
Pamoja na mambo mengi, alisema sheria hiyo imeweka mambo mbalimbali na maamuzi mengi yaliyokuwa yafanywe na waziri mwenye dhamana hiyo sasa yatakuwa yakishughulikiwa na Baraza Huru la Habari Tanzania.
Awali kabla ya kumkaribisha waziri, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga aliwataka waandishi wa habari kuisoma sheria hiyo kwa makini na kuielewa ili watekeleze majukumu yao kulingana na matakwa halisi ya sheria husika.
Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), Absalom Kibanda alidai sheria hiyo ilipitishwa haraka huku maeneo mengi yakiwa na upungufu na hawakupata nafasi ya kufanya marekebisho na kusema miaka 10 iliyopita, ilikuwa ya serikali ya kiza.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Hassan Abbas aliyesema sio kweli miaka 10 iliyopita ilikuwa ya serikali ya giza kwani kila utawala uliopita ilitekeleza jambo fulani.
“Sio kweli serikali iliyopita ilikuwa ya kiza, kesho (leo) tunasherehekea miaka 55 ya Uhuru, kila utawala uliopita ulitekeleza jambo fulani katika kusaidia nchi kuendelea,” alisema Abbas na kubainisha kuwa awamu ya kwanza, ilijihusisha na ujenzi wa nchi mpya, kujenga misingi ya taifa; awamu ya pili iliboresha miundombinu ya nchi na demokrasia; awamu ya tatu iliimarisha misingi ya kisera, kisheria na kitaasisi wakati awamu ya nne ilijenga uchumi na kuimarisha miundombinu.
Alisema hizo zote ni juhudi za kuijenga nchi na kauli kuwa awamu iliyopita ilikuwa ya kiza sio sahihi kwani mengi ya kimaendeleo yalifanywa na awamu ya tano inaendeleza kwa kuimarisha uchumi na kuhakikisha dira ya maendeleo ya mwaka 2025 inatekelezwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Media Foundation (TMF), Ernest Sungura alisema taasisi yake itafadhili mikutano ya waandishi wa habari nchi nzima ili waifahamu sheria hiyo, lakini pia kutoa maoni yao kuhusu kutungwa kwa kanuni za sheria hiyo ya habari.
0 Maoni:
Post a Comment