Mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge la 9 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samuel Sitta unatarajiwa kuagwa leo mchana na wabunge wa Bunge hilo katika viwanja vya Bunge vya mjini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa mjini hapo na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alipokuwa akitoa ratiba ya kuuaga mwili wa spika mstaafu itakayoanza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za Bunge za kipindi cha asubuhi.
Mhe. Ndugai amesema kuwa Bunge linatarajia kuupokea mwili wa mpendwa huyo leo mnamo majira ya saa 8 mchana kutoka katika uwanja wa ndege wa Dodoma na kupelekwa moja kwa moja ndani ya Bunge hilo kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho na wabunge.
“Baada ya mwili wa mpendwa wetu kuwasili katika viwanja hivi, tutakuwa na kikao maalum cha Bunge kitakachofanyika mida ya saa 8:30 mchana ambapo wabunge watapata nafasi ya kutoa salamu za rambirambi na baadaye utaratibu wa kutoa heshima za mwisho utafuata”, alisema Mhe. Ndugai.
Spika Ndugai ameongeza kuwa baada ya utoaji wa heshima za mwisho utakaoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe, kwa mwili wa marehemu Samuel Sitta utasafirishwa kwa ndege mnamo majira ya saa 10 jioni kwenda wilaya ya Urambo, mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Novemba 12 mwaka huu.
Aidha, Mhe. Ndugai amefafanua kuwa katika msiba huo Bunge litawakilishwa na wabunge 10 watakaochaguliwa na Tume ya Huduma za Bunge kwa kuzingatia uwakilishi wa vyama ukiongozwa na yeye Spika Mhe. Ndugai kwenda mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi.
Kutokana na msiba huo, Mhe. Ndugai amesema kuwa Bunge litajenga misingi ya kuwaheshimu viongozi wa kitaifa wanaopatwa na jambo la namna hiyo kwa kupewa heshima hizo za kuletwa Bungeni kwa ajili ya kuagwa kwa msingi wa Bunge kuwa ndio nyumba ya uwakilishi wa Watanzania wote.
0 Maoni:
Post a Comment