Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS ), Omar Said Shaaban amemshauri Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein asiusaini Muswada wa sheria ya mafuta na gesi uliopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hivi karibuni kwa madai kuwa unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Omari ameeleza msimamo huo katika barua yake ya maneno 1,293 aliyomwandikia Dk Shein akifafanua jinsi gani muswada huo unavunja sheria na Rais huyo anavyoingizwa kwenye mtego wa kuvunja Katiba.
Katika barua hiyo, mwanasheria hiyo anasema, “Mheshimiwa Rais, zipo taarifa kuwa unajiandaa kuweka saini kwenye muswada huo uliopitishwa na Baraza la Wawakilishi ili hatimaye iwe sheria. Naomba nikunasihi uachane na mpango huo ili kujiepusha na mtego wa jaribio la kuvunja Katiba.”
Anasisitiza, “Kwa heshima naomba nikueleze kuwa jaribio la Serikali yako na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na hatua yako ya kuweka saini muswada huo ili uwe sheria, ni uvunjaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo wewe umeapa kuilinda, lakini pia ni kinyume na maelekezo ya sheria inayorejewa kama ndiyo chanzo cha mamlaka ya Zanzibar kutunga sheria yake.”
Mwanasheria huyo anabainisha kuwa kama kweli nia ya dhati ipo ya kuondoa mafuta na gesi kwenye Muungano, hatua pekee na salama kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kusukuma kumalizika kwa mchakato wa Katiba Mpya au kupelekwa mabadiliko ya Katiba Bungeni kuliondoa jambo hilo kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.
Omari alisema akiwa mwanasheria tena kiongozi kwenye kada hiyo, ana wajibu wa kikatiba, kimamlaka na kitaaluma kusimamia ulindwaji na usimamizi wa Katiba na sheria za nchi na akiwa mwenye uchungu na Zanzibar, anapenda kuona ikisimamia rasilimali zake yenyewe bila ya kukiuka masharti ya Katiba.
Alibainisha kuwa katika Katiba ya Muungano kwenye nyongeza ya kwanza, suala la mafuta na gesi ni jambo la Muungano hivyo usimamizi wake na utungiwaji sheria kwa mujibu wa Katiba zote mbili upo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hakuna mahali duniani kote ambapo suala lenye misingi yake kikatiba linaondolewa kwa “makubaliano ya viongozi wa wakuu wa Serikali,”anasema.
0 Maoni:
Post a Comment