KULIKUWA na haraka gani ya Kamati ya utendaji ya klabu ya Simba SC kuitisha mkutano wa dharura wa mabadiliko ya katiba mwezi ujao? Kuna sababu gani ya Simba kujiingiza katika presha ya ‘Dar es Salaam-Pacha’ wakati huu?
Na ni nani anayewaendesha viungozi wa Simba kwa ‘rimonti’ akiwa nyumbani kwake? Bado unaamini Simba inakwenda kushinda ubingwa wake wa kwanza wa ligi kuu baada ya kupita misimu minne?
Baada ya mechi 13 pasipo kupoteza msimu huu, stori ya Simba kurudia historia yao wenyewe-kumaliza msimu pasipo kupoteza mechi ilitawala.
Labda kwa kutokufahamu, kukumbuka, ama kujua kwamba msimu wa 2009/10, Patrick Phiri akiongozwa na uongozi wa Mzee Hassan Dalali kama Mwenyekiti, Mwina Kaduguda kama Katibu Mkuu wa kuchaguliwa na wajumbe makini katika kamati ya utendaji, waliisaidia Simba kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania Bara kushinda ubingwa wa ligi kuu pasipo kupoteza game hata moja kati ya michezo 22 (wakati huo ligi kuu ikichezwa na timu 12).
Msimu wa 2007/08 ambao ulikuwa ni wa kwanza baada ya Shirikisho la kandanda nchini-TFF kufanya marekebisho ya kalenda yake ya michuano. VPL iliyokuwa ikichezwa kuanzia mwezi Februari/Machi na kumalizika Oktoba/Novemba hadi kufikia mwa 2006. Mwaka 2007, TFF ilianzisha ligi kuu ya mpito ili kupata wawakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya Caf 2008.
Simba ilishinda ubingwa huo baada ya kuishinda Yanga SC kwa changamoto ya mikwaju ya penalti katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Simba ilishinda ubingwa huo baada ya mahasimu wao Yanga kufanya hivyo mara mbili mfululizo miaka ya 2005 na 2006.
Msimu wa kwanza VPL kuchezwa kuanzia Agosti/Septemba na kumalizika April/Mei ni ule wa 2007/08. Baada ya Abuu Mtiro kushindwa kufunga mkwaju wa penalti ya mwisho ambayo ingeipa Yanga taji la tatu mfululizo la VPL katika fainali ya ‘ligi kuu ndogo 2007,’ Yanga ikatoka chini ya msimamo na kufuta gepu la pointi 11 kati yake na Tanzania Prisons na kushinda ubingwa msimu wa 2007\08.
Wapinzani wa Yanga walikuwa Prisons na hadi sasa sielewi ni kwanini Prisons haikushinda ubingwa ule wakati nafasi ilikuwa yao. Walikuwa na timu bora kama ile ‘iliyoshindwa’ kupata sare tu ili kuwa mabingwa wa VPL mwaka 2002 mbele ya Yanga pale Sokoine Stadium.
Usidhani Simba ilikuwa na kikosi dhaifu. Simba ilikuwa kali mno, lakini iliyumbishwa na migogoro iliyokuwa ‘ikitengenezwa nje ya uongozi’ na baadhi ya wanachama waliokuwa na ndoto ya kuongoza klabu hiyo baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Dalali na Kaduguda walikuwa wakichonganishwa na watu wenye pesa na maelewano yao hafifu wakati fulani yaliiangusha sana Simba ndani ya uwanja. Phiri alifanya nao kazi akaondoka, Mbrazil, Neidor dos Santos akaingia naye akashindwa.
Ilifikia wakati fulani katika game vs Yanga, kocha Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ akatumika kama ‘kiraka wa muda’ na Boniface Pawassa akasimama kwenye benchi kama kocha msaidizi, na bado Yanga walipigwa pale Jamhuri Stadium, Morogoro.
Kina Dalali walilazimika kufanya kazi na makocha wengi ndani ya muda mfupi kutokana na makocha hao kushindwa, na walishindwa kwa sababu klabu haikuwa na pesa huku wachezaji muhimu wakilipwa na baadhi ya wafanyabiasha wanachama wa klabu.
Mbrazil, Nelson Eliasi pia alipita katika timu hiyo , huyu anaweza kuwa kocha aliyedumu Simba kwa muda mfupi zaidi. Baadae akaja, Mserbia, Milovan Curkovic lakini naye akashindwa na chini yake nidhamu ya kawaida na hata ile ya kimchezo kwa wachezaji wake ikashuka kwa kiwango kikubwa sana na timu ikamaliza katika nafasi ya tatu msimu wa 2007/08.
Mlinzi wa kati, Mkenya, George Owino akajiunga na Yanga kama mchezaji huru , mlinzi wa pembeni, Nurdin Bakary naye akajiunga Yanga kama mchezaji huru, golikipa bora zaidi wa karne mpya Tanzania na ‘hirizi ya bahati klabuni Simba,’ Juma Kaseja naye akajiunga na Yanga kama mchezaji huru. Wanachama wengi na mashabiki wakachanganyikiwa.
Wote hao wakaenda kuisaidia Yanga kushinda ubingwa wake wa nne wa VPL ndani ya misimu mitano (2005, 2006, 2007/08 na 2008/09).
Phiri aliporejea akahitaji utulivu klabuni na akasuka kikosi bora na kikashinda ubingwa pasipo kupoteza mchezo wowote msimu wa 2009/10.
Phiri alipata matokeo baada ya uongozi kumaliza tofauti zao na kusaidiana naye kuhakikisha wanamaliza ufalme wa Yanga ‘ambao hauna mwisho katika soka la Tanzania Bara.’
Phiri alimshawishi Kaseja kurejea Simba akafanikiwa. Nico Nyagawa, Musa Hassan Mgosi, Ulimboka Mwakingwe ni baadhi ya wachezaji waliomsaidia Phiri na klabu kushinda ubingwa.
Wote ukiwauliza watakwambia, walifanikiwa baada ya utulivu hata pale waliposhindwa kupata ushindi katika game muhimu dhidi ya timu kama Villa Squad na Polisi Dodoma. Umakini mdogo katika uongozi ndio ulianza kuiangusha timu na kushindwa kutetea ubingwa kwa tofauti ya goli moja dhidi ya Yanga msimu wa 2010/11.
Yanga ilitoka nyuma ya pointi 9 dhidi ya Simba katika game 6 za mwisho na kutwaa ubingwa wake wa tano ndani ya misimu 7.
Ni umakini huohuo na utulivu katika uongozi ndio unaendelea kuwaangusha Simba hadi sasa. Msimu uliopita walionekana kama wanaenda kushinda ubingwa baada ya kuwa mbele kwa alama 7 dhidi ya Yanga na Azam FC lakini wakajiingiza katika presha kufuatia kugomea kuendelea kucheza game zao hadi Yanga na Azam walingane katika idadi ya michezo.
Azam walihangaika sana kufuta gepu la pointi 7 na Yanga walipambana haswa huku pointi 9 wakizipata baada ya kutoka nyuma ya goli 1-0 vs Mwadui FC (uwanja wa Taifa), 1-0 vs JKT Mgambo (uwanja wa Taifa) na 1-0 vs Toto Africans (uwanja wa Kirumba,) Mechi zote walishinda 2-1 baada ya dakika 90 na wakafuta gape la pointi kati yao na Simba na kwenda kileleni ambako hawakushuka tena.
Simba waliporejea kucheza wakawa juu ya Azam FC lakini chini ya Yanga kwa alama 2. Wakachapwa na Toto 1-0 (uwanja wa Taifa) kisha wakapoteza 1-0 vs Mwadui (uwanja wa Taifa).
Kwa kasi waliyokuwa nayo na tamaa ya ubingwa iliyowaingia ghafla wangeendelea kushinda kila mchezo kama wangeendelea kucheza mechi zao na Yanga wasingeweza kufuta tofauti ya pointi 13 hadi 16 kama wangecheza game tatu tu mbele zaidi ya pale walipogomea.
Safari hii baada ya kupoteza michezo miwili ya mwisho kati ya 15 katika raundi kwanza, kiongozi mmoja akakimbilia katika media na kuwaambia wanahabari ‘wawaambie’ walimwengu kwamba kuna wachezaji wao wana wahujumu-Pigo la kwanza katika ndoto zao za ‘alinacha’ ya ubingwa msimu huu.
Majuzi nimesikia wakitangaza mkutano wa dharura wa klabu mapema mwezi ujao. Nimeshangaa sana kwa kweli! Mbona uongozi huu wa Simba unajipeleka katika nyakati ngumu wao wenyewe wakati muda wao mgumu katika ligi haujawafika?
Nadhani mkutano wa mabadiliko wa katika ya Simba ungefanyika Juni 2017 na si mwanzoni mwa mzunguko wa pili ili waendelee kuwa wamoja. Katika ligi yoyote timu bingwa hupitia wakati mgumu, na Yanga wameshapita katika kipindi chao kigumu katika ligi, Simba wanajiwahisha.
Mkutano wa dharura wakati si wote wanaafiki ni njia nyingine yakuongeza mpasuko-Pigo la pili katika ndoto zao za ‘alinacha’ ya ubingwa msimu huu.
Juzi tena, sijui Haji Manara katokea wapi, anasema hawataingiza timu yao uwanjani kucheza na Yanga ikiwa waamuzi watatoka hapa Tanzania! Hawa Simba wanashangaza sana, mbona wanafungwa kila msimu na Prisons lakini hawajaomba waamuzi wa kigeni.
Huu ni uoga mkubwa kuwahi kuoneshwa na Simba dhidi ya Yanga. Nawashauri Ndanda FC, Ruvu Shooting, JKT Ruvu nao wapeleke barua TFF wakiomba game zao vs Simba wawagharamikie waamuzi wa kigeni ili wapate matokeo sahihi. Kwani wakichezeshwa na waamuzi wa Bara kila game wanapoteza?-Pigo la tatu katika ndoto zao za ‘alinacha’ ya ubingwa msimu huu.
0 Maoni:
Post a Comment