Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la John Mtemi (23) amejinyonga baada ya kumuua mke wake Casta Edward kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi amesema tukio hilo lilitokea Machi 26 saa sita mchana katika Kijiji cha Mahaha, Kata ya Shishani wilayani Magu.
Kamanda Msangi amesema tukio hilo limegundulika baada ya mwenye nyumba waliyokuwa wakiishi Daudi Philipo kupita nje ya nyumba hiyo na kuona damu zikiwa zimechuruzika nje ya mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi wanandoa hao.
“Polisi wamekuta mwili wa mwanamke upo mlangoni lakini ilionekana michirizi ya damu kutoka chumbani, na polisi walipoingia chumbani walikuta mwili wa mwanaume ukining’inia kwenye waya wa umeme,” amesema Msangi.
Amesema chanzo cha mauaji bado hakijafahamika licha ya kudaiwa kuwa wanandoa hao walikuwa wakiishi kwa amani bila ugonvi wowote na kwamba uchunguzi bado unaendelea.
Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa ajili ya uchunguzi na ukikamilika itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Kamanda huyo amewataka wana ndoa kutojichukulia sheria mkononi na kuomba wananchi waendelee kutoa taarifa za uhalifu.
0 Maoni:
Post a Comment