JESHI LA POLISI LAKANA KUHUSIKA NA KIFO CHA MFANYABIASHARA MBEYA

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limesema kuwa halihusiki kwa namna yoyote na kifo cha mfanyabiashara ya machungwa, Allen Mapunda (20) anayedaiwa kufariki muda mfupi baada ya kuachiwa na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga amewaeleza waandishi wa habari kuwa, jeshi hilo halihusiki na kifo hicho na kwamba amefungua jalada la uchunguzi kupitia ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumzia tukio hilo, alisema kuwa Machi 24, mwaka huu saa sita usiku, askari polisi waliokuwa katika operesheni ya kukamata wahalifu katika mtaa wa Airport kata ya Iyela jijini hapa waliwakamata vijana 12 akiwemo Allen.
Mpinga alisema Machi 25, mwaka huu saa nne asubuhi alitoka mahabusu baada ya kudhaminiwa na ndugu zake na ilipofika saa 12 jioni zilipatikana taarifa kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.
Alisema baada ya taarifa hizo wananchi wa Airport walifanya vurugu na kuharibu nyumba ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Boaz Kazimoto wakimtuhumu kuwa yeye ndiyo aliwaita polisi.
Alisema wananchi hao waliendelea na vurugu hizo kwa kuvunja madirisha na kuharibu samani za ofisi ya kata na baadaye kuchoma moto meza za wafanyabiashara.
“Lakini pia walivamia nyumba ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia mwenye namba H.4325 PC Yohana kuvunja madirisha na kutishia kuichoma moto," alisema.
Alisema polisi walipofika kutuliza ghasia, wananchi hao walirusha mawe na kuvunja kioo cha mbele cha gari la polisi lenye namba za usajili PT 1987 aina ya Toyota Land Cruiser na polisi kulazimika kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo kuwatawanya na kwamba kutokana na tukio hilo wanawashikilia watuhumiwa nane.
Aliwataja watu wanaowashikilia kuwa ni Bariki Masoud (30), Frank Kilemi (33), Eliud Daudi (22), Krist Nelson (33), Estom Mbalo (24), Robert Mwangupili (24), Issa Nelson (26) na Felix Mbilinyi(21) wote wakazi wa Kata ya Iyela Jijini Mbeya.
Juzi mama mdogo wa narehemu, Alice Mapunda alinukuliwa na waandishi wa habari kuwa akiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda Nyanda za Juu Kusini, madaktari walimueleza kuwa inaonekana Allen alikuwa amepigwa sana na kwamba kila sehemu anayoguswa analalamika kupata maumivu.
"Kabla ya kuondoka kituo cha polisi tuliomba watupatie fomu namba tatu ya polisi (PF3), lakini askari aliyekuwepo alituhoji atupe ya nini wakati kijana huyo anaumwa ugonjwa wa Mungu tu," alisema.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment