Mlinzi, mfanyakazi benki mbaroni shambulio la Meja Jenerali mstaafu


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kutokana na kupigwa risasi kwa Meja Jenerali mstaafu Vincent Mribata akiwemo mlinzi wa nyumba yake, Godfrey Gasper pamoja na mfanyakazi wa Benki ya NBC, tawi la Tangibovu katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Meja Jenerali Mribata alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 11, mwaka huu, wakati anaingia getini nyumbani kwake Tegeta na kukimbizwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo ambako amelazwa akipatiwa matibabu. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema Meja Jenerali Mritaba alivaamiwa na watu wawili wasiojulikana na kumjeruhi kwa kumpiga risasi mkononi, tumboni na kiunoni na kumpora kiasi cha Sh milioni tano.

Alisema shambulio hilo lilitokea baada ya kutoka kuchukua fedha Benki ya NBC Tangibovu akiwa kwenye gari yake aina ya Volkswagen Amarok yenye namba za usajili T 443 DDH. Aliongeza kuwa alipofika nyumbani kwake alipiga honi na kufunguliwa geti na mlinzi wake ambaye ni askari wa Suma JKT, geti lilipofunguliwa pikipiki ilisimama getini na watu wawili waliokuwa wamevaa kofia ngumu walishuka na kulifuata gari hilo huku wakiwa na silaha aina ya bastola.

Alisema mlinzi huyo alikamatwa kwa kuwa aliiacha silaha yake wakati akifungua geti na wakati wa tukio hilo likitokea mlinzi alikimbia nje ya uzio akiacha bunduki yake aina ya shotgun yenye namba TZCAR 96444 kwenye kibanda cha ulinzi. “Haiwezekani askari umepata mafunzo ya kijeshi, lakini unatoka kufungua geti silaha unaacha kibandani na jambazi anakuamuru uondoke na unaondoka hata hujapigwa ngumi moja lazima tufuatilie tubaini ukweli,” alisema Kamanda Mambosasa.

Aliongeza kuwa mtumishi huyo wa benki alikamatwa kwa kuwa imebainika kulikuwepo kwa mawasiliano yaliyofanywa na mtumishi huyo kwenda kwa mtu mwingine, hivyo jeshi linamshikilia ili kuwabaini wote waliohusika katika tukio hilo. Katika tukio jingine, jeshi hilo limesema linaendelea na upelelezi ili kuwabaini watu waliohusika na tukio la kuvamiwa kwa Ofisi ya Mawakili ya Prime.

Alisema baada ya taarifa za kuvamiwa kupokewa askari walifika eneo hilo la tukio kwa ajili ya ukaguzi na ufuatiliaji ambapo walimkuta Hudson Ndusyepo (53) wakili wa kampuni hiyo na kufanya naye mahojiano pamoja na watu wengine watatu ambao ni mlinzi wa jengo hilo kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Liganga.

Kamanda Mambosasa alisema mlinzi huyo alieleza kuwa akiwa lindoni, walifika wanaume watatu ambao walimvamia kumfunga kamba miguuni na plasta mdomoni na ghafla waliongezeka kufikia wanane na hatimaye kuvunja mlango na kuingia ndani.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment