Mapema leo bodaboda na Bajaji walikusanyika ofisini kwa mkuu wa
mkoa wa Iringa Mhe. AMINA MASENZA
kukabidhi madawati kama msaada ambao umelenga kutatua tatizo la madawati katika
baadhi ya shule Mkoani Iringa.
Madawati hayo kumi na sita(16) yenye thamani ya shilingi Laki tisa
na elfu sitini (960,000) yamekabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Iringa ofisini kwake
huku akipewa jukumu la kuchagua shule yenye upungufu wa madawati ili kuweza
kuyapeleka.
Akikabidhi madawiti hayo mwenyekiti wa Bodaboda na Bajaji Manispaa ya Iringa Joseph Mwambope amesema ni
kawaida yao kama chama cha Bodaboda kutoa msaada pale ambapo wanaguswa, kama vile waliweza kutoa unga wa sembe kwa
wafungwa gerezani na sasa wameamua kutoa madawati hayo kwaajili ya kuwasaidia
wanafunzi.
Sambamba na hilo mwenyekiti Mwambope amemuomba mkuu wa mkoa wa
Iringa kuwatafutia eneo la kufanyia kazi Katikati ya mji ambapo kuna abiria
wengi lakini hawana eneo kwaajili ya kupaki bajaji zao ili waweze kufanya
biashara zao.
“Sisi kama Bodaboda na Bajaji hatuna ugomvi na Polisi wala SUMATRA
ila kuna watu wasio na malengo mazuri dhidi yetu wamekuwa wakijaribu
kuwagombanisha ili wao waonekane kuwa ni wabaya kwa polisi na SUMATRA”. Alisema
Mwambope.
Akipokea Msaada huo wa madawati kutoka kwa vijana wa bodaboda
Manispaa ya Iringa Mheshimiwa Amina Masenza amewashukuru kwa kupata msaada huo
ambao umekuja kwa wakati muafaka na wakati ambapo yanahitajika.
“Nashukuru kwa msaada wenu ila Madawati haya moja kwa moja
nayapeleka Wilayani Kilolo ambapo kuna uhitaji mkubwa wa madawati kwani hapa
manispaa Hakuna shida kubwa sana ya madawati”. Alisema Masenza.
Masenza amewaomba vijana hao chini ya mwenyekiti wao Mwambope
kuweza kutii sheria na kanuni za barabarani ili kuepusha ajali kwani wengi wao
wamekuwa wakaidi wa sheria hizo.
“Ninawaombeni muweze kujiunga na Mfuko wa bima ya afya pindi
mtakapopata ajali muweze kujitibu wenyewe na kuondokana na gharama za
matibabu”. Aliongeza Masenza.
0 Maoni:
Post a Comment