WAZAZI wa wanafunzi Mugisha Lukambu na Atuganile Jimmy ambao ni miongoni
mwa wanafunzi 10 wa mchepuo wa sayansi wamebainisha kuwa walilazimika
kuwajengea misingi mizuri watoto wao tangu wakiwa na umri mdogo baada ya
kubaini kipaji chao
Mugisha (Feza Boys) na Atuganile (Feza Girls) ni miongoni mwa wanafunzi 10 bora wa masomo ya sayansi katika matokeo ya Kidato cha Sita ambao katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2014 walikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Musoma, baba mzazi wa Mugisha, Reynold Lukambuzi alisema mtoto wao alionesha kipaji akiwa mdogo jambo ambalo liliwasukuma kumpeleka shule mapema.
Mugisha na Atuganile ni miongoni mwa nwafunzi 10 bora wa masomo ya sayansi katika matokeo ya Kidato cha Sita ambao mwaka 2014 katika matokeo ya kidato cha nne walikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa.
Mugisha aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Bendel Memorial alishika nafasi ya tano, wakati Atuganile aliyemaliza Shule ya Sekondari ya Canossa alishika nafasi ya nane. Akizungumza na gazeti hili kutoka Musoma, Lukambuzi ambaye ni mwalimu mstaafu alisema, “Mugisha alikuwa na kipaji, alikuwa na uwezo wa kupambanua mambo makubwa tofauti na umri wake, jambo ambalo lilitusukuma kumpeleka shule mapema akiwa na umri wa miaka mitatu.”
Alisema ili kuendeleza kipaji chake, yeye na mzazi mwenzake Yustina Lukambuzi, waliamua kumpeleka kwenye shule za kulipia wakiamini ndio shule ambazo zingeweza kumjenga na kuendeleza kipaji chake. Alisema alipata elimu ya msingi katika shule ya Emmanuel iliyopo Musoma mjini ambako alifanya vizuri na baadaye kumpeleka shule ya kulipia ya Bendel Memorial iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro ambako alimaliza elimu ya kidato cha nne.
Mugisha ambaye katika matokeo ya kidato cha sita akiwa amepanda nafasi moja hadi kuwa nafasi ya nne ukilinganisha na yale ya kidato cha nne, kwa sasa yuko kwenye mafunzo ya hiyari ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Songea.
Alisema kutokana na kufanya vizuri akiwa kidato cha nne, Mugisha alipata fursa ya kusomeshwa miaka miwili bure katika Shule ya Sekondari ya Feza Boys jijini Dar es Salaam akichukua masomo ya tahasusi ya PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia).
“Kwa kweli tumepokea matokeo kwa furaha kubwa, kipaji chake ndicho kilichotufanye tumepeleke shule za private, na ndicho kilichofanya asomeshwe bure kwa miaka miwili na Shule ya Sekondari ya Feza,” alisema.
Naye baba mzazi wa Atuganile aliyechukua masomo ya tahasusi ya PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati), Cairo Jimmy alisema “Tumefurahi kwa mwanetu kwanza kushirikilia namba ile aliyoipata kwenye matokeo ya kidato cha nne. Ni binti ambaye anapenda kusoma na mara nyingi amekuwa akinisimbua kwa kuhitaji vitabu mbalimbali vya kujisomea.”
Aliongeza: “Tulichofanya sisi kama wazazi ni kumuwekea msingi mzuri wa somo la hisabati tangu akiwa darasa la kwanza, na tushukuru naye aliitikia mwito kwa kusoma vizuri na kupenda sana Hisabati.
“Mimi nilikuwa mzuri kwenye hesabu kwenye shule ya msigi na sekondari kidogo, lakini Atuganile alikuwa ni wa pekee kwani hata mimi wakati mwingine alinizidi jambo ambalo lilinifanya nimtafute raifiki yangu (Twahili Mshana),” alisema.
Alisema Atuganile aliyemaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mwangaza iliyopo Gongo la Mboto, Ilala alifaulu vizuri na kupangiwa shule ya wanafunzi wenye vipaji ya Tabora.
“Alipangiwa Tabora, lakini tuliamua tujifunge mikanda na kujibana ili akasome Canossa ambako aliongoza katika kipindi chate cha masomo yake,” alisema. Alisema baada ya matokeo ya kidato cha nne, alifuatwa na uongozi wa Feza ambao walitaka akasome katika shule hiyo.
“Kwa sababu Atuganile aliongoza Mkoa wa Dar es Salaam walipokuwa wakipewa zawadi, Feza walitufuata, lakini si unajua shule hizo ada yao ni kubwa, lakini wao walitaka akasome na kutupunguzia ada kutoka shilingi milioni tisa hadi kulipa shilingi milioni 1.5 kwa mwaka,” alieleza.
Jimmy ambaye yeye ni mhasibu, alisema awali mtoto wao walimshauri akasomee udaktari kutokana na kushika nafasi ya tatu kwenye somo la baolojia, lakini aligeuka na kukataa kusoma PCB kwa madai hakuna hesabu.
“Awali tulikubaliana akasome udaktari, lakini alivyoenda Feza alisema atasoma PCM kwa sababu PCB haikuwa na hesabu, na yeye alitaka kuendelea na hesabu zake, lakini sasa amebadili mtazamo na kutaka kujihusisha na masuala ya ndege,” alifafanua mzazi huyo.
Kwa upande wake, uongozi wa Shule ya Sekondari ya Mwenyeheri Anuarite umeeleza sababu zilizowaweka kwenye kundi la shule 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka huu ikiwemo kuwa darasa la kwanza kuhitimu kidato cha sita na nidhamu hafifu kwa baadhi ya wanafunzi.
Aidha, umesema pia kuwa pamoja na kuwa nafasi ya nne katika kundi hilo jambo lililowashtua na wao baada ya kusikia matokeo hayo, lakini kiuhalisia wahitimu katika shule hiyo walikuwa 30 na kati yao, wanafunzi sita ndio waliopata sifuri na watatu daraja la nne.
Waliopata daraja la tatu ni 15, la pili ni watano na daraja la kwanza ni mmoja. Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Mkuu wa Shule hiyo inayomilikiwa na Parokia ya Mtakatifu Gaudence, Makoka, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Carlos Mgumba alisema wamejifunza kutokana na makosa kadhaa yaliyojitokeza ikiwemo ndio wahitimu wa kwanza wa kidato cha sita kwa shule hiyo.
“Kuna mambo kadhaa tumejifunza kutokana na uchanga wetu wa darasa hili la kwanza kuhitimu kidato cha sita kwetu mwaka huu. Wengi wa wanafunzi wetu hapa ni wa mchepuo wa sanaa na wote wamefaulu vizuri,” alisema Mgumba.
Alisema wanafunzi wote waliopata sifuri ni wa mchepuo wa sayansi na wengi wao ni waliogoma waliposhauriwa kubadilisha mchepuo tangu wakiwa kidato cha tano baada ya kuonekana ufaulu wao si mzuri katika eneo la sayansi.
Mwalimu Mgumba alisema walianza wakiwa na wanafunzi 13, lakini wengine walihamia na kuongeza changamoto ya kuwa na uelewa mmoja tofauti na walioanza na walimu tangu awali.
Akifafanua zaidi kuhusu sababu za kufanya vibaya, alisema kuna baadhi ya wanafunzi waliibuka na kuwa na tabia zisizoridhisha na walipofikiria kuwapumzisha nyumba (ni shule ya bweni) kama walivyofanya shule nyingine za kanisa, waliona sababu ni darasa la kwanza la elimu ya juu ya sekondari (A Level), watawavunja moyo na kuwaacha lakini wengi ndio waliofeli.
“Hakuna mwanafunzi aliyesikiliza mwalimu vizuri darasa, amefeli, kuna walioshauriwa kubadili mchepuo baada ya kuonekana masomo waliochagua, hawawezi na waliokubali, wamepata daraja la pili na la tatu,” alisema Mgumba.
Kuhusu umahiri wa walimu, Mgumba alisema ana ujasiri wa kusimama popote kuelezea umahiri mkubwa wa walimu waliopo katika shule hiyo kwa uzoefu wa ufundishaji, elimu zao, shule walizofundisha ambazo baadhi ni za kanisa zilizopo katika 10 bora na nidhamu kubwa ya kazi pamoja na idadi yao kukidhi mahitaji.
Alisema kwa wastani kwa kidato cha tano na cha sita, kila somo linafundishwa na walimu wawili na maabara ina vifaa vyote kwa ajili ya masomo ya sayansi. Hata hivyo, alisema ili kuondoa sifuri katika shule yao, alikutana na wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu na walimu kuwatia moyo ili wajitambue kuwa wanaweza kufanya vizuri zaidi na matokeo si ya kusitisha hivyo yasiwakatishe tamaa.
Alisema kama shule, wamejizatiti kuongeza mitihani ya majaribio kila wiki kwa wanafunzi wa kidato cha sita, wameanzisha kitengo cha ushauri wa masuala ya elimu na binafsi kwa wanafunzi ili wawe huru kujieleza wanapoona kuna tatizo na ushauri hufanywa na watu wa nje ili wawe huru kujieleza.
Wakizungumzia matokeo na namna walivyojipanga kufanya vizuri katika mitihani yao, Kaka Mkuu wa Shule, Teophily Mbiro anayesoma PCB, alisema walipokea kwa huzuni matokeo ya wenzao na wamekutana na mkuu wa shule na walimu na kukubaliana kutorudia makosa ya wenzao.
Shule zilizo katika kundi la 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Jumamosi ambayo wasichana waliongoza kwa ufaulu na idadi ya wanafunzi katika shule hizo kwenye mabano ni Kiembesamaki, Unguja (120), Hagafilo, Njombe (53), Chasasa, Pemba (76), na Mwenyeheri Anuarite, Dar es Salaam (30).
Nyingine ni Ben Bella, Unguja (108), Meta, Mbeya (300), Mlima Mbeya, Mbeya (59), Njombe, Njombe (455), Al-Ihsan Girls, Unguja (41) na St Vicent, Tabora (31). Imeandikwa na Gloria Tesha na Anastazia Anyimike.
0 Maoni:
Post a Comment