MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amefanya tena mabadiliko katika jeshi hilo.
Katika mabadiliko hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, SACP Suzan Kaganda amekuwa Mkuu wa Kitengo cha Mafao na Fidia katika Makao Makuu ya Jeshi hilo huku nafasi yake ikichukuliwa na ACP Jumanne Murilo ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi hilo, ACP Barnabas Mwakalukwa kwa vyombo ya habari jana, nafasi ya Kamanda Murilo imechukuliwa na ACP Simon Haule aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa Mkoa wa Mara.
Mwakalukwa amesema mabadiliko hayo ni ya kawaida katika kuboresha utendaji kazi. Mwanzoni mwa mwezi huu, IGP Sirro ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo Februari mwaka huu, alimteua ACP Mwakalukwa kuwa msemaji mpya wa jeshi hilo akichukua nafasi ya Kamishina Msaidizi, Advera Bulimba ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Katika mabadiliko mengine yaliyofanywa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga aliteuliwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mnadhimu wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Fortunatus Musilim. Naye aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alihamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi.
0 Maoni:
Post a Comment