WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.
Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alisema serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.
“Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo,” alieleza Majaliwa. Alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evangelical Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Rais John Magufuli.
Alisema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi. Spika wa Bunge, Job Ndugai alimpa pole Dk Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo wakati wa uhai wa marehemu Linah.
0 Maoni:
Post a Comment