Vituo vya mafuta vyaonja joto TRA

Kituo cha Mafuta
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza operesheni ya kuvamia vituo vya mafuta na jana imewatoza faini wenye vituo ya mafuta kiasi cha Sh milioni 4.5 kwa kila kituo ambacho kilikutwa hakitoi stakabadhi wakati kinapofanya malipo.

Vituo ambavyo TRA ilivivamia jana ni vituo vitatu vya Oil Com Makumbusho, Victoria na Oil Com cha Kijitonyama, vyote vya Dar es Salaam na vilikutwa vikiuza mafuta bila kutoa stakabadhi na kupigwa faini ya Sh milioni 4.5 kila kimoja.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi huo, Meneja Elimu kwa Walipa Kodi, Daina Masala alisema kwamba wanafuatilia vituo ambavyo havijafunga mashine za malipo za kielektroniki (EFDs) kwenye pampu ya mafuta baada ya kudokezwa kuwa baadhi ya vituo hivyo vimekuwa havitoi stakabadhi.

Alisema hata mtu ambaye anaweka mafuta kwenye gari lake, akikamatwa na TRA akitoka kwenye kituo cha mafuta bila kuwa na stakabadhi, atapigwa faini ya kati ya Sh 30,000 na Sh milioni 1.5.

Alisema licha ya elimu kubwa kutolewa na TRA juu ya matumizi ya EFDs, anashangaa bado kuna wafanyabiashara ambao wanajaribu kukwepa kodi na akaonya kuwa wenye tabia hiyo waache mara moja.

Aliwashutumu baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa baadhi yao waliomba wasifunge mashine hiyo moja kwa moja kwenye pampu kutokana na gharama kuwa kubwa na TRA ikaridhia kwamba kwa kipindi ambacho bado wanaendelea kujadiliana wawe wanatumia mashine za EFD kutoa stakabadhi ya malipo.

TRA imefanya operesheni hiyo kutokana na kuwepo madai ya baadhi ya vituo vya mafuta kutotoa stakabadhi jambo ambalo linaikosesha serikali mapato. Kisheria ni kosa kwa mtu kununua au kuuza kitu bila kudai au kutoa stakabadhi ya malipo.

Masala alisisitiza kuwa wataendelea kufanya operesheni hizo za kushtukiza katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwabaini wote wanaojaribu kukwepa kulipa kodi halali ya serikali.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment