Hakimu
Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili
Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Godbless Lema dhidi ya
Rais Dkt Magufuli amejitoa baada ya upande wa Jamhuri kusema kuwa hawana
imani naye.
Wakili
wa Serikali Sabina Silayo alisema kuwa hawawezi kusoma hoja za awali za
kesi hiyo kwani hawana imani na hakimu huyo kutokana na kuwa na
urafiki na mke wa mtuhumiwa, Godbless Lema jambo ambalo linaweza
kuathiri mwenendo wa kesi na haki isitendeke.
Licha
ya kuwa upande wa utetezi ulilipinga hilo wakisema kuwa haina uzito na
kwamba watanzania wote ni marafiki na ndugu, lakini hakimu huyo
aliridhia kujiondoa katika kesi hiyo ambayo inatarajiwa kuendelea tena
Agosti 8 mwaka huu ambapo hoja za awali zitasomwa huku jalada
likipelekwa kwa Hakimu Mfawidhi ili apangiwe hakimu mwingine.
Hakimu
huyo ni wa pili kujitoa katika kesi hiyo, kwani Mei 29, Hakimu Mkazi wa
Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha pia alijitoa kwa maelezo kuwa hawezi
kusikiliza kesi zote nne zinazomkabili Lema hivyo kuwaeleza mahakimu
wengine watapangiwa kesi hiyo.
Wakili
wa Lema, Shedrack Mfinanga aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo
kutokana na mteja wake kutokuwapo mahakamani kwani anaumwa.
0 Maoni:
Post a Comment