Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, jana
tarehe 3 Julai, 2017 amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya
siku mbili na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela
pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza.
Akiwa
mkoani hapa Mhe. Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa
mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini
Sengerema leo tarehe 4 Julai, 2017.
Katika
Uwanja wa Ndege wa Mwanza Mhe. Rais Dkt. Magufuli alikutana na kamati
ya amani ya viongozi wa dini na kuwashukuru viongozi hao kwa sala na
dua zao na amewataka waendelee kuwahimiza waumini wao kuliombea Taifa
ili liepukane na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa maendeleo.
Akiwa
njiani kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza katika eneo la Bwiru kuelekea
Ikulu ndogo ya Mwanza, Mhe. Rais Magufuli msafara wake ulisimamishwa
mara kwa mara na wananchi waliojaa barabarani na kuamua kuzungumza nao
ambapo aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepania kupambana
na ufisadi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali
tofauti za dini au Siasa.
Aidha,
aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali yake imedhamiria kuondoa
kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi zenye kero na
kuwapatia vitambulisho wafanyabishara wadogo wadogo, maarufu kama
Wamachinga, ili waweze kufanya biashara zao bila kusumbuliwa.
Akiwa
eneo la Nyamagana jijini Mwanza, Mheshimiwa Rais alitembea kwa miguu
huku kuwasalimu wananchi waliokuwa wakimshangilia na kuzuia msafara
wake.
Rais
Magufuli pia alikwenda Uwanja wa Mpira wa Nyamagana na kuungana na
baadhi ya wananchi waliokuwa wakiangalia mechi ya mpira wa miguu kati
ya timu ya Buhongwe na Nyamwaga.
Mhe.
Rais Dkt. Magufuli pia amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara
ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi katikakati ya jiji ambao
gharama za ujenzi wake zilitokana na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa
ajili ya sherehe za Muungano.
Jaffar Haniu Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
0 Maoni:
Post a Comment