KOCHA Juma Mwambusi amesema kwamba hatafundisha timu yoyote msimu huu kufuatia kuondoka Yanga baada ya kumaliza mkataba wake.
Akizungumza
na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Mwambusi amesema kwamba dhamira
yake ni kujiondoa kwenye shughuli za mpira kwa muda ili ashughulikie
mambo yake mengine binafsi.
Mwalimu
huyo wa zamani wa Moro United, Prisons na Mbeya City, amesistiza kwa
ushawishi wowote hata wa fedha ikitokea timu inataka kumrudisha kwenye
mpira msimu huu, atashikilia msimamo wake wa kupumzika.
“Mimi
nimemaliza mkataba Yanga na sijaongeza, kwa sababu dhamira yangu ya
muda mrefu ni kupumzika kwa msimu huu ili nifanye mambo yangu
binafsi,”amesema.
Mwambusi amesema msimu ujao atarejea kwenye mpira baada ya kukamilisha jukumu analotaka kulifanya kwa sasa.
Mwambusi amefanya kazi Yanga kwa misimu miwili kama kocha Msaidizi, kwanza chini ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na baadaye Mzambia, George Lwandamina aliye kazini kwa sasa.
Kocha huyo Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 akiwa na Mbeya City ya nyumbani kwao, Mbeya alifanya kazi kwa maelewano mazuri na ‘wakubwa’ zake wote, Pluijm na Lwandamina.
Na Bin Zubeiry Sports – Online inaamini Yanga inaachana na Mwambusi tu kwa sababu za kuyumba kiuchumi, kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wake, Yussuf Manji.
Kwa sasa anayekaimu Ukocha Msaidizi wa Yanga ni beki na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele, aliyekuwa kocha wa kikosi cha vijana cha wana Jangwani hao.
Lakini
habari zaidi zinasema Yanga inataka kumchukua kocha wa Kagera Sugar,
Mecky Mexime kuwa Mwalimu Msaidizi wa kikosi cha kwanza na Nsajigwa
aendelee na kazi ya kutengeneza vipaji Yanga B.
0 Maoni:
Post a Comment