Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu
limetangaza kuwa, wahajiri wapatao 44 ambao wengi wao ni kutoka nchi za
magharibi mwa Afrika wamefariki dunia kwa kiu kaskazini mwa Niger baada
ya lori walilokuwa wakisafiria kuharibika katikati ya jangwa.
Afisa
wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika mji wa Bilma nchini Niger
amewaambia waandishi wa habari kwamba, wahajiri hao waliopoteza maisha
wengi wao ni raia wa Ghana na Nigeria. Lawal Taher amesema kuwa,
miongoni mwa wahajiri waliofariki dunia katika ajali hiyo wamo watoto
wawili wadogo na kwamba, sita kati yao wamenusurika kifo.
Taarifa
zaidi zinasema kuwa, wahajiri sita walionusurika kifo walilazimika
kutembea kilomita kadhaa hadi kufika katika kijiji kimoja na kuomba
msaada wa maji na chakula.
Hata
hivyo hadi sasa viongozi wa serikali ya Niger bado hawajathibitisha
habari hiyo. Wimbi la wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya kutafuta
maisha bora limeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na
kwamba baadhi hufanikiwa kufika salama huko waendako, lakini hadi sasa
idadi kubwa ya wahamiaji hao haramu wamepoteza maisha katika safari hizo
za kuelekea barani Ulaya.
0 Maoni:
Post a Comment