SIMBA leo ina kazi nyingine ngumu itakaposhuka kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam kumenyana na Stand United katika mechi ya Ligi Kuu Bara. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kulingana na mahitaji ya timu zote mbili na Simba ikipoteza maana yake inajiondoa kwenye mbio za ubingwa, hivyo hiyo ni karata yake ya mwisho.
Simba ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 62 sawa na Yanga inayoongoza kwa uwiano mzuri wa mabao, inapewa nafasi kubwa ya kushinda, kutokana na malengo ya kutaka kuwavua ubingwa Yanga ingawa kwa idadi ya mechi walizobakiwa nazo ukilinganisha na Yanga wanahitaji miujiza. Hiyo ni mechi ya 29 kwa Simba endapo watashinda watafikisha pointi 65 na kurudi kileleni kwa muda kwani kesho Yanga itacheza na Mbeya City na ikishinda itarudi tena kileleni kwa uwiano mzuri wa mabao.
Matumaini ya Simba kuendelea kuwepo kwenye mbio za kuwania ubingwa ni kushinda mechi ya leo, lakini ikiomba Yanga kesho ivurunde licha ya kwamba jambo hilo ni gumu. Kocha wa Simba Joseph Omog, amesema mchezo wa leo wameupa umuhimu hivyo pamoja na kuwa na nafasi ndogo ya ubingwa lakini watapambana ili kuhakikisha wanashinda mechi zao mbili zilizosalia. “Nitatumia kikosi kamili kwasababu ligi bado inaendelea na japo nafasi ni ndogo ya ubingwa lakini hizi ni mbio lazima tupambane hadi dakika ya mwisho kwani mpinzani wetu anaweza kupoteza ikawa faida kwetu,” alisema Omog.
Pia Omog alisema kikosi chake hakitakuwa na mabadiliko makubwa na kile kilichocheza mchezo uliopita dhidi ya African Lyon, ambao walishinda kwa mabao 2-1. Kocha wa Stand United Athuman Bilal ametamba kuyeyusha ndoto za Simba kuwania ubingwa. Bilali alisema hawawezi kukubali kupoteza mchezo huo kwani hata wao wapo katika hali mbaya na wanahitaji pointi tatu ili kujiweka salama na janga la kushuka daraja msimu huu.
“Ni mchezo mzuri na mgumu timu yangu imejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na utakuwa na ushindani lakini tunahitaji pointi tatu au ikishindikana basi tupate hata moja naamini itatusaidia kuondoka katika janga la kushuka daraja,” alisema Bilali. Pia Bilali alisema amekuja na nyota wake wote akiwemo Adam Kingwande, Amri Kiemba na Jacob Masawe hivyo anatarajia kutoa presha kubwa kwa wapinzani wao Simba ambao wataingia kwa nguvu ya kutaka mabao ya mapema.
Mchezo mwingine leo utakuwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi ambapo wenyeji Azam FC wataialika Toto Africans ya Mwanza. Mchezo huo ni muhimu kwa Toto ambayo ipo kwenye ukanda wa kushuka daraja ikiwa na pointi 29 kwenye msimamo wa ligi katika nafasi ya 15. Fainali na Juventus ni maalumu - Zidane
0 Maoni:
Post a Comment