MBEYA City imesema haitaki kuwa ngazi ya Yanga kutwaa ubingwa hivyo watahakikisha hawapotezi mechi ya kesho kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika mechi ya raundi ya kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, timu hiyo iliibuka kidedea dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, Yanga. City iliweka kambi Sumbawanga ambapo imedai kambi ya huko inatosha kuwamaliza wapinzani wao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha wa Mbeya City Kinna Phiri alisema mchezo wao dhidi ya Yanga utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao hao kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao, lakini hawatakubali kuwa ngazi. “Tumefanya maandalizi mazuri na tumerudi kutoka Sumbawanga, ambako tuliweka kambi ya siku tano na kucheza michezo minne ya kirafiki, ambayo tulishinda yote,” alisema Phiri.
Pia alisema wanaendelea na mazoezi makali kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mechi ya kesho watakayohakikisha wanarudi Mbeya na pointi tatu. “Sisi tunachotaka ni kuwafunga tu, haijalishi kama hatuwi mabingwa au hatushuki. Tunataka kulinda heshima kwa kuwafunga mabingwa watetezi itakuwa heshima nzuri kwani hatutaki kuwa ngazi ya ubingwa ya Yanga,” alisema. Mbeya City inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza michezo 28.
0 Maoni:
Post a Comment