Mauaji ya kutumia silaha yanaendelea kujitokeza wilayani
Rufiji mara baada ya kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amiri Chanjale
mkazi wa Umwe ,tarafa ya Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani kuuawa kwa
kupigwa risasi kichwani na watu wasiojulikana.
Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Njwayo amesema tukio hilo
limetokea usiku wa kuamkia leo wakati marehemu akiwa amepumzika nyumbani
kwake.
Amesema kuwa watu hao walifika nyumbani kwa marehemu na
kuingia ndani kisha kumfyatulia risasi ya kichwa hali ambayo
ilimsababishia maumivu makali ambayo yalipelekea kupoteza uhai na watu
hao kutokomea kusikojulikana.
“Jeshi la polisi bado linaendelea na kazi yake ya
kuwasaka wauaji na mtandao wao wote, hivyo niwatoe hofu wananchi kuwa
kila kitu kinaanza taratibu, na Serikali itashinda kwani hakuna
linaloshindikana,”amesema Njwayo.
Kwa upande wake Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Onesmo Lyanga, amesema kuwa polisi bado inaendelea
na kazi yake usiku na mchana kuwasa na kuhakikisha wanaukamata mtandao
wote unaohusika na mauaji hayo.
Hata hivyo, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo
amewatoa hofu wananchi wa maeneo hayo na kusema kuwa Jeshi la Polisi
linaendelea na operesheni yake ya kuhakikisha mtandao wa wahalifu hao
unatokomezwa.
0 Maoni:
Post a Comment