KATIKA kuadhimisha miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais John Magufuli (pichani) amesamehe wafungwa 2,219 wakiwemo wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na wale wenye ulemavu wa akili, lakini kwa sharti kuwa maradhi hayo lazima yathibitishwe na jopo la madaktari.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Projest Rwegasira haikutaja idadi ya wafungwa hao, lakini ilifafanua kuwa miongoni mwa wafungwa waliosamehewa ni wale ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya Kifungu 49 (1) cha Sheria ya Magereza, wawe wametumikia nusu ya vifungo vyao vilivyobaki. Wafungwa wengine waliosamehewa na Rais Magufuli ni wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, na saratani ambao wako kwenye “terminal stage”.
Taarifa ilisisitiza kuwa wafungwa hao wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya. Wengine waliosamehewa ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, lakini umri huo unatakiwa pia uthibitishwe na jopo la madaktari. Pia wamo wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Wengine waliosamehewa ni wale wenye ulemavu wa mwili na akili, lakini ulemavu wao pia uthibitishwe na madaktari. “Wafungwa 2,219 watafaidika na msamaha huu na wataachiliwa huru. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” ilisema taarifa hiyo ya Meja Jenerali Rwegasira.
Msamaha huo wa Rais hawauwahusu wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo na wale waliofungwa baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka yao. Pia msamaha huo hauwahusu wezi wa pikipiki, magari na wale waliofungwa kwa kuharibu miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo. Katika orodha hiyo, Rais pia hakuwasamehe wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu na wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa msamaha huo wa Rais, hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani au wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Rwegasira alifafanua kuwa wengine ambao hawako kwenye msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kama vile kokeni, heroin, bhangi na mirungi.
Kwenye orodha hiyo wamo wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa. Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo na wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali.
Rais Magufuli pia hakuwasamehe wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo. Wengine ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea.
“Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo. Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii,” ilisema taarifa hiyo ya Rwegasira. Rwegasira katika taarifa yake alisema wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na wale waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki, pia hawamo kwenye msamaha huo.
Wamo wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili, wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali. Wengine ni wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali na wafungwa walioingia gerezani baada ya Machi 16, mwaka huu na wale wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani.
0 Maoni:
Post a Comment