BAADHI ya wanaume katika Kata ya Chipanga katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, wanadaiwa kuwasumbua wanawake wanaopata fedha zinazotolewa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) wakitaka mahusiano nao ili wanaume hao wafaidi pesa hizo; imefahamika.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika vijiji vya Chali Msanga na Chali Makulu katani hapo wakati wa ugawaji fedha zinazotelowa na Mfuko huo, baadhi ya wanawake walisema baadhi ya wanaume wakiwamo wenye ndoa na familia zao wanapoona fedha hizo zimetoka huwapa wakati mgumu kwa kuwafuata fuatakutokana na wao kutokuwa na fedha.
Happy Masaka (20) mkazi wa Kijiji cha Chali Msanga alisema amekuwa akiishi kwa kusumbuliwa na waume wa watu anapopokea fedha hizo hali ambayo imekuwa ikimkosesha raha.
Alisema wanaume hao wakisikia fedha za Tasaf zimetoka wanajipanga ili kuhakikisha wanawarubuni.
“Kunakuwa na usumbufu mkubwa, mimi nishafuatwa na wanaume wanne tena wote wana wake zao inakuwa usumbufu pamoja kuwa bado sijaolewa, lakini siwezi kuchukua mume wa mtu na wanafanya vile ili tuwape pesa hizo,’’ alisema.
Naye Cecilia Isume (28) Mkazi wa Kijiji cha Chali Makulu alisema kwa upande mwingine, fedha za Tasaf zinapotolewa baadhi ya wanawake hususan ambao hawajaolewa, nao hujipodoa na kujipitishapitisha kwa wanaume wanaopokea fedha hizo ili kuwatia vishawishini.
‘’Hata wadada, nao wakijua pesa za Tasaf zimetoka, utawaona wanavaa vizuri na kujipodoa ili kuwachuna hao wanaume,’’ alisema.
Musa Matonya Kijiji cha Chali Makulu alisema baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia vibaya pesa hizo kwa kuamini pesa ndiyokila kitu ili kuwapata wanawake jambo ambalo sio sahihi kwa kuwa hawajui malengo ya pesa hizo.
“Unakuta wanaume wanataka dogodogo hivyo wanaamua kutumia fedha hizo ili wawapate kwa urahisi. Hii ni mbaya sana,’’alisema.
Mratibu wa Tasaf Wilayani Bahi, Joseph Kileo alisema baada ya kubaini kuwa baadhi ya wanaume wanatumia vibaya pesa hizo, walitoa maelekezo fedha zichukuliwe na mkuu wa kaya ambaye ni mama.
0 Maoni:
Post a Comment