POLISI mkoani Morogoro imeendelea na operesheni ya kupambana na dawa za kulevya na ‘kamatakamata’ ya pombe kali zilizo katika vifungashio vya plastiki ‘viroba’ vilivyopigwa marufuku na imewakamata watu 25.
Kati ya watuhumiwa hao, 14 wamekamatwa kwa kukutwa na pombe kali katika vifungashio vya viroba na 11 dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema mjini hapa kuwa watuhumiwa hao 11 walikamatwa katika matukio tofauti yaliofanyika Machi 8, mwaka huu saa 7 usiku katika kijiji cha Singisa tarafa ya Bwakila wilaya ya Morogoro.
Alisema kati ya watuhumiwa hao 11, watano waliokamatwa wakijiandaa kusafirisha bangi hiyo katika viroba 31 vyenye ujazo wa kilogramu 50 kwa kila kiroba kwenye pikipiki mbili tofauti, bangi iliyochambuliwa kwa ajili ya matumizi kilo tatu, misokoto 641 iliyokuwa tayari kutumiwa na miche ya bangi 26.
Alisema watuhumiwa hao waliwakamatwa wakijiandaa kuisafirisha bangi hiyo kwa kutumia pikipiki mbili namba MC 880 BLT aina ya King Lion na T 478 BWH aina ya Sanya kutoka kijiji cha Singisa, kwa ajili ya kusambaza sehemu za mikoa mbalimbali nchini.
Pia katika operesheni hiyo Polisi inamshikilia mtuhumiwa mmoja baada ya kukamatwa na pombe aina ya moshi ‘gongo’ lita 18 aliyokuwa ameificha uvunguni mwa kitanda chake.
Kuhusu operesheni maalumu dhidi ya pombe kali za viroba, ambavyo vimepigwa marufuku kwa jina la ‘viroba’ iliyofanyika Machi 3, mwaka huu alisema kuwa jumla ya watuhumiwa 14 walikamatwa.
Kamanda huyo wa mkoa alisema kuwa watuhumiwa wao, walikamatwa na viroba ambavyo ni katoni 128, dazeni 117 na pakiti 16 za pombe aina valeur, zedi, nguvu, spirit, kiroba original, konyagi na vodka vikiwa na ujazo wa milimita 50 na 100.
Kwa mujibu wa kamanda, watuhumiwa wote hao wanaendelea kuhojiwa na hatua za kuwafikisha mahakamani zinafuata.
Matei alitoa onyo kali kwa wote wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya na pombe kali na kuwataka kuacha mara moja, kwani Jeshi la polisi lipo mahali popote.
0 Maoni:
Post a Comment