Magufuli, Museveni pamoja bomba la mafuta



RAIS John Magufuli ameitaka Kampuni ya Total inayowekeza katika ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, kuacha visingizio na kuanza ujenzi wa bomba hilo mara moja.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais Magufuli alisema serikali imeshughulikia masharti yote saba ambayo mwekezaji hayo aliyataka.

“Masharti aliyoyataka kwa upande wa Tanzania yameshashughulikiwa yote ikiwa ni pamoja na suala la msamaha wa kodi ya thamani. Hivyo hili si tatizo tena, mhusika aambiwe asitafute visingizio vidogovigo vya kushindwa kujenga halafu akasingizia mahali fulani hawafanyi kumbe yeye ni tatizo.

Alisema pia serikali imetoa fursa nyingi kwa mwekezaji huyo ili kurahisisha kazi yake ya ujenzi wa bomba hilo huku akisisitiza kama kuna mambo madogo madogo yanajitokeza yashughilikiwe huku ujenzi ukiendelea.

Rais Magufuli alisema katika kuonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, Serikali imeshaanza upanuzi wa bandari ya Tanga ili kuwezesha shughuli za ujenzi wa bomba hilo kwenda vizuri.

“Tanzania tuna uzoefu na masuala ya ujenzi wa mabomba, hili litakuwa bomba la tatu kujengwa kwani kuna bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Zambia (TAZAMA) na lile la la gesi asili (kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam),” alisema.

Aliongeza; “Tumeamua tuwakubalie ndugu zetu waganda, kwa sababau waganda ni ndugu zetu, masuala mazuri ya Uganda ni lazima tuyapokee sisi kwa mikono miwili na ndio maana nimemhahakikishia rais kuwa bomba lilitakiwa lianze kujengwa jana kwa sababu sisi hatuna tatizo.”
Rais Magufuli alisema hata maeneo ambayo bomba hilo litapita ambayo ni ya hifadhi ya barabara, Serikali itahakikisha inalitatua hilo ili kuhakikisha bomba hilo linapita na kujengwa.

Rais Museveni baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu suala la ujenzi wa bomba la mafuta, aliahidi kufuatilia baadhi ya mambo kwa upande wa nchi yake ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kama ulivyopangwa.

“Tumegundua mafuta mwaka 2006 hata kabla ya Ghana, lakini kwa muda mrefu yamebaki ardhini kwa sababu kuna baadhi ya makampuni makubwa yalitaka kufanya udanganyifu wa njia ya kipitisha mafuta.

“Hatimaye sasa tumepata njia ya kupitisha mafuta, hivyo hatuna sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa sababu utatupa fedha ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu na kuibadili kabisa nchi yetu,” alisema.

Aidha, viongozi hao wawili wamekubaliana mwekezaji huyo kuanza mchakato wa kuhakikisha jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo haraka iwekezenavyo.

Rais Museveni ameishukuru serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi miwili ya umeme ambayo itasaidia vijiji vilivyoko Tanzania na vile vya Uganda kupata umeme wa uhakika.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment