Rais
John Magufuli amekataa shule ya msingi iliyojengwa hivi karibuni eneo
la Bunju, Wilaya ya Kinondoni kuitwa kwa jina lake badala yake ameagiza
iitwe kwa jina la Mkuu wa wilaya hiyo, Ally Hapi. Taarifa ya badiliko la
jina haikutolewa na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kama
ilivyozoeleka bali na mkuu wa wilaya hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi
vifaa mbalimbali vya usafi kwa uongozi wa shule hiyo. “Shule hii
imejengwa kwa fedha zilizopatikana baada ya Serikali
Kuu kubana matumizi. Tukaamua iitwe John Magufuli lakini yeye akatoa
agizo shule ipewe jina la mkuu wa wilaya sina budi kukubaliana na
hilo,”alisema Hapi. Shule hiyo mpya iliyopo Bunju jijini imejengwa kwa
lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Bunju A
ambayo ilikuwa na wanafunzi 3,224.Mwalimu mkuu wa shule hiyo mpya, Ali
Mwakapalila alisema ingawa inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9
mwakani inakabiliwa na changamoto mbalimbali. “Hakuna umeme wala maji,
hii inaweza kuleta madhara kwa wanafunzi hasa linapokuja suala la
matumizi ya vyoo,” alisema.
Baada
ya hafla hiyo, Hapi alikwenda kwenye kiwanda cha saruji cha Twiga
Cement ambako alipokea msaada wa mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya
kufanikisha ujenzi wa madarasa na majengo mengine.
Akipokea
msaada huo, Hapi alisema msaada kutoka Twiga Cement unaunga mkono
juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoipa sekta ya elimu kipaumbele
ili kuhakikisha inatolewa katika mazingira bora. “Msaada huu umekuja
muda muafaka. Tumeshajenga shule ila tunataka kuongeza madarasa,
maabara, ofisi ya elimu na kuzungushia uzio ili watoto wawe katika
mazingira salama. Lengo ni kuifanya shule hii iwe ya kisasa na itakuwa
mfano kwa shule zote za Wilaya ya Kinondoni,”alieleza.
Pia,
Hapi alisema wilaya hiyo ipo kwenye mipango ya kujenga maktaba ya
kisasa kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya saruji. Mkurugenzi Mtendaji
wa Twiga Cement, Alfonso Velez alisema kuchangia katika shughuli za
kijamii ni moja ya mambo ambayo wamekuwa wakiyapa kipaumbele zaidi.
“Kushiriki
shughuli za maendeleo katika jamii ni jambo ambalo tunalipenda zaidi.
Yalipo maendeleo Twiga Cement ipo pia,” alisema Velez.
0 Maoni:
Post a Comment