Wanawake, watoto mbaroni vitendo vya ugaidi

Kamanda Saimon Sirro Akionesha vitu vilivyoibwa

POLISI Kanda Maalumu Dar es Salaam kupitia kikosi kazi kinachopambana na uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi, kimewakamata wanawake wanne na watoto wanne kwa tuhuma za kujihusisha na mafunzo ya ugaidi katika maeneo ya Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema watoto hao wanne walikuwa wametoroshwa kutoka familia ya Shabani Abdala Maleck ambaye ni mkazi wa Kitunda.
Kamanda Sirro alisema polisi ilipokea taarifa kutoka kwa mzazi mmoja wa kiume aitwaye Maleck, kuwa ametoroshewa watoto wanne na mtalaka wake aitwaye Salma Mohamed aliyeingizwa kwenye harakati za kigaidi.
Alisema wawili hao walitengana Februari mwaka huu na Juni mwaka huu, mwanamke huyo ndiyo alikwenda Kitunda na kuwatorosha watoto hao.
Alisema kati ya watoto hao waliokamatwa mmoja imebainika kuwa ni wa Maleck.
“Jitihada za pamoja kati ya mtoa taarifa na Polisi zilifanikisha kuwakamata wanawake wanne na watoto wanne katika eneo la Kilongoni Vikindu mkoani Pwani wakiwa wamekusanywa kwenye nyumba ya mtu mmoja anayeitwa Suleiman, wakiwa wanafundishwa mambo ya dini na harakati za kigaidi,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema baada ya mahojiano zaidi na watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, imejidhihirisha kuwa baadhi ya watoto hao wameachishwa masomo katika shule mbalimbali nchini.
“Baadhi ya watoto wameachishwa na wazazi na walezi wao na kuingizwa katika madrasa ambazo ndizo kambi walikokamatiwa chini ya uangalizi wa wanawake waliokamatwa pamoja nao,” alifafanua.
Alisema sanjari na mafunzo ya madrasa, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu ikiwemo karate, kung-fu na judo na kufundishwa jinsi ya kutumia silaha aina ya SMG na bastola.
Pia alisema wanafundishwa kupiga maeneo tete ya kummaliza mtu pumzi na kufariki haraka wakati wa mapigano (pressure point) ili kumdhibiti adui, kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe.
“Watoto hao wamefundishwa kuwa adui yao mkubwa ni Polisi, walinzi katika taasisi za fedha na makafiri katika kujipatia kipato, wamefunzwa kupora au kunyang’anya kwa kutumia silaha na kutumia viungo vyao,” aliongeza.
Alisema wanawake hao na watoto wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao mzima katika suala hilo ili kutokomeza tabia hiyo ya kuwaachisha watoto wadogo shule na kuwaingiza katika vitendo vya uhalifu.
Katika tukio lingine, Padri wa Kanisa Katoliki Sumbawanga, Destrious Apolinary anashikiliwa kwa tuhuma ya kuwa na gari ya wizi lenye namba T 616 DCH Toyota Land Cruiser mali ya Joseph Kayawaya iliyoibwa jijini Dar es Salaam, kughushiwa na kuuzwa jijini Arusha.
Mtuhumiwa anahojiwa na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, Kamanda Sirro alisema wamewakamata watuhumiwa watano wa ujambazi katika maeneo ya Tuangoma baada ya kupatikana na mali ya wizi ambayo iliporwa kwa nguvu nyumbani kwa Patrick Samari (35), mfanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Kitengo cha Biashara.
Akizungumzia tukio hilo, alisema kundi la watu wapatao 15 walimvamia Samari nyumbani kwake na kuvunja mlango kwa matofali na kuingia ndani na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo bastola yenye usajili A731441 ikiwa na risasi 12 ndani ya magazini yake.
Pia waliiba fedha taslimu Sh 10,180,000, televisheni inchi 54, Laptop mbili aina ya HP na simu mbili za mkononi aina ya Samsung.
Alisema baada ya taarifa hizo polisi walianza kufanya kazi ya ufuatiliaji na kuwakamata Penza Seleman, Mwarami Nasoto, Sweed Shabani, mkazi wa Kinondoni Manyanya, Mussa Ismail, mkazi wa Sinza na Salum Taidini.
Alisema watuhumiwa wote hao walikiri kuhusika na tukio hilo na mali zote za wizi walidai walihifadhi kwa Tadini na baada ya mahojiano zaidi na upekuzi vilipatikana vifaa vyote vilivyoibwa pamoja na gari namba T 533 DEQ aina ya Toyota TI inayotumika kubeba mizigo sehemu wanazoiba. Upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment