Sasa ICC yaiandama Marekani

Fatou Bensouda Pressekonferenz (picture-alliance/dpa)
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inasema ina sababu za kimsingi kuamini kuwa wanajeshi wa Marekani wamefanya matendo ya uhalifu wa kivita na hivyo kuashiria kuwepo uwezekano wa kuwafungulia mashitaka.
Katika ripoti yake ya awali, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, amesema kuwa kwa uchache kuna visa 61 vilivyorikodiwa, ambapo matukio ya utesaji, ukatili na kuvunja heshima ya watu yanahusika. Ripoti hiyo pia inataja visa vyengine 27 vya watu walioteswa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) vingi vyao vikitokea baina ya mwaka 2003 na 2004. 
Ripoti hii iliyotolewa Jumatatu (14 Novemba) inahoji kwamba uhalifu unaodaiwa kutendeka haukuwa matukio yaliyojitenga kando, bali ni sehemu ya mbinu zilizothibitishwa na Marekani katika majaribio ya kupata taarifa kutoka kwa mahabusu.
"Kuna ushahidi wa kutosha kuamini kuwa uhalifu huu ulitendeteka katika kuendeleza sera ya kupata taarifa kupitia matumizi ya mbinu za mahojiano zinazojumuisha njia za kikatili au fujo, ambazo zingelisaidia malengo ya Marekani nchini Afghanistan." Bensouda anasema kwenye ripoti hiyo.
Marekani yakanusha 
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Elizabeth Trudeau, amesema nchi yake haiamini kuwa uchunguzi wa ICC umeidhinishwa au unafaa.
"Marekani imejitolea kweli kweli kwenye kuheshimu sheria za vita, na tuna mfumo wa kitaifa wa uchunguzi na uwajibikaji ambao unakidhi viwango ya kimataifa kwa kila hali," alisema Trudeau mara baada ya ripoti ya Bensouda kuwekwa hadharani.
USA Donald Trump (Getty Images/S. Olson)
Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameapa kwamba atarejesha mbinu zote za kikatili katika kuwalazimisha "magaidi" kutoa taarifa zitakazosaidia kuilinda Marekani dhidi ya mashambulizi.
Naye msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Kapteni Jeff Davis, alisema maafisa wa jeshi wanangojea kupata ufafanuzi juu ya madai hayo ya ICC kabla ya kutoa kauli yao. 
Mahakama hii iliyoanzishwa mwaka 2002 kwa ajili ya kuendesha kesi za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya halaiki, inasema itaamua hivi karibuni ikiwa iendeshe uchunguzi kamili dhidi ya wanajeshi wa Marekani ama la. 
Akiwa wakati huo mgombea urais kwa tiketi ya Republican, Rais mteule wa Marekani Donald Trump alisema mapema mwezi huu wa Novemba, kwamba atarejesha mbinu ya kuadhibu kwa kutumia maji na mbinu nyengine mbaya zaidi ya hiyo katika kuwalazimisha "magaidi" kutoa taarifa. 
Ingawa Marekani kamwe haijawahi kusaini mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo ya ICC, lakini kwa kuwa visa vinavyotajwa vimetendeka katika ardhi za mataifa mengine, kama vile Afghanistan, Poland, Lithuania na Romania, ambazo ni wanachama wa ICC, mahakama hiyo inayo nguvu za kisheria kuvichunguza. 

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alisaini Mkataba wa Roma tarehe 31 Disemba 2000, lakini mrithi  wake, George Bush aliikataa sahihi hiyo, akidai kuwa Wamarekani wasingelitendewa vyema kwenye mahakama hiyo kwa sababu za kisiasa.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment