Polisi wafanya msako dhidi ya 'IS' Ujerumani

Symbolbild Salafismus (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)
Polisi wa Ujerumani wamefanya msako kwenye majimbo 10 hapa Ujerumani katika msako dhidi ya wanachama wa kundi la Kiislamu la DWR wanaoendeleza shughuli za kuwasajili wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani kundi hilo la DWR  "Die wahre"  kwa maana kwamba ni "Dini ya kweli" ni mtandao unaondeleza maslahi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS ingawa msemaji huyo amefahamisha kuwa kundi hilo halijaonyesha mpaka sasa ishara zozote za kutaka kufanya mashambulio ya kigaidi humu nchini.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere anaamini kuwa kundi hilo limekiuka katiba ya Ujerumani na kwamba linaendeleza uchochezi na chuki miongoni mwa watu.  Waziri huyo anatarajiwa kutoa tamko maalum baadaye leo.  hadi tunapokwenda hewani hakuna taarifa zozote kutoka kwenye kundi hilo. mbali na taarifa fupi kwenye mtandao wa Twitter inayosema kuwa "Quran imekatazwa Ujerumani" na kuendelea kusema "tumefikisha ujumbe wa Allah"
Wakati huo huo Polisi huko mjini Berlin wamefanya msako katika maeneo karibia 200,ikiwemo misikiti, ofisi na makaazi ya watu wanaoshukiwa kuwa ni wanachama wa kundi hilo la DWR  ambalo linajulikana hapa nchini kwa kusambaza na kugawa Quran na vilevile kwa mpango wao wenye utata unaoitwa "Lies" yaani Soma!
Wataalamu wa maswala ya dini wanasema kuwa nakala za tafsiri ya Quran zinazosambazwa na kundi hilo ni tofauti na maandiko asili yaliyo katika lugha ya Kiarabu. Imani ya Masalafisti inaelekeza kuwa na msimamo mkali wa dini ya Kiislamu pamoja na kutumia sheria kali kushinikiza mambo. 
Wizara ya mambo ya ndani imeeleza sababu ya kufanywa kwa msako huo katika hotuba kwa waandishi wa habari kwamba Quran hiyo inatumiwa na kundi la DWR kuendeleza chuki na kwamba takriban vijana 140 wameshasafirishwa hadi nchini Syria na Irak kujiunga na makundi ya Jihad. Msako huo umefanywa wiki moja baada ya serikali kuanza kumsaka kinara wa mtandao wa Masalafist hapa Ujerumani Abu Walaa mwenye umri wa miaka 32 raia wa Irak ambaye yupo hapa nchini tangu mwaka 2000.  Anatuhumiwa kwa kuliunga mkono kundi la Dola linalojiita la Kiislamu IS.
Deutschland PK Thomas de Maizière zu Großrazzia in zehn Bundesländern (picture-alliance/dpa/R. Jensen)
Msako katika eneo la Magharibi mwa Ujerumani umewahusisha mamia ya maafisa wa polisi huku uchunguzi wa kitengo cha intelijensia ya ndani ya nchi umeeleza  kwamba kundi hilo linatukuza kundi la IS pamoja na Jihad huku likijishughulisha na usajili wa wapiganaji wapya ambao wanapelekwa nchini Syria na Irak kwenda kujiunga na kundi la wapiganaji wa IS.  Takriban  majimbo 10 yakiwemo North Rhine- Westphalia, jimbo la Kaskazini la Hamburg na jimbo la Kusini la Baden-Wuerttemberg yamepitiwa na msako wa polisi.  Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Hesse Peter Beuth amesema polisi wamefanya msako katika eneo lake pia ameongeza kusema  kuwa vitendo vya kuwachochea vijana na kisha kuwapeleka kujiunga na makundi ya Jihad kamwe havikubaliki.
Wizara ya mambo ya ndani imeeleza kuwa kwa kulipiga marufuku kundi hili itakuwa ni njia mojawapo ya kulitokomeza kabisa nchini kote na kwamba wale wanoeneza chuki hawatapewa nafasi ya kujificha chini ya mwavulii wa uhuru wa kuabudu.
Share on Google Plus
Ahsante kwa kutembelea site yangu, unaweza kunicheki kwenye mitandao ya kijamii kwa kubonyeza icons juu kulia na kunipata moja kwa moja kwenye Facebook, Twitter na Instagram...Endelea kuwa karibu yangu ili uweze kufikiwa na chochote kinachonifika.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment