TAKRIBANI siku 10 tangu kupitishwa kwake na Mkutano wa Tano wa Bunge la 11, Rais John Magufuli ametia saini Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kwa vyombo vya habari jana, Rais Magufuli amesaini sheria hiyo juzi Novemba 16, 2016.
“Dk Magufuli amewapongeza wadau wote kwa kufanikisha kutungwa kwa sheria hiyo,” ilisema taarifa ya Ikulu.
“Naamini kuwa sheria hii itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa manufaa ya wanataaluma wenyewe na Taifa,” amesema Rais Magufuli, kwa mujibu wa Ikulu.
Kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo, kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau kuhusu muswada huo wakitaka Bunge liahirishe kuujadili hadi Februari mwakani ili kupata nafasi zaidi ya kuusoma, na wakaenda mbali zaidi ya kumwomba Rais Magufuli asiusaini kuwa sheria.
Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika kutimiza mwaka mmoja madarakani Novemba 4, mwaka huu, Rais Magufuli alisema atausaini mara tu utakapofikishwa kwake kwa sababu hawezi kuingilia kazi za mhimili mwingine wa dola (Bunge).
Rais alisema sheria yoyote hupelekwa bungeni, kutokana na misingi yake na mahitaji yake na kwamba Sheria ya sasa ya Huduma za Habari, imeanza kupelekwa bungeni tangu mwaka 2011, lakini mara zote imekuwa ikipigwa danadana.
Akifanya majumuisho ya hoja kabla ya muswada kupitishwa bungeni Novemba 5, mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema umezingatia mabadiliko ya teknolojia na ndiyo sababu sasa mmiliki wa mtambo wa kuchapia magazeti, hataadhibiwa pindi gazeti linapokuwa na habari yenye makosa, isipokuwa pale itakapothibitika amehusika kwa makusudi.
Alisema muswada huo umemlinda mwanahabari kwa kumlazimisha mmiliki wa chombo cha habari, kutoa mikataba ya ajira, kumkatia bima ya mazingira magumu na ya afya na kuwepo chombo cha mafunzo cha kuwaendeleza wanahabari, tofauti na zamani ambapo alisema ‘wakijiendeleza wenyewe kama kuku wa kienyeji’.
Akitetea zaidi muswada huo ulivyomsaidia mwanahabari, alisema litakuwepo Baraza Huru la Habari, litakaloundwa na wanahabari wenyewe na hakutakuwa na mkono wa waziri.
“Baraza halitapewa fedha na serikali, hivyo litakuwa huru, si sasa MCT (Baraza la Habari Tanzania) ni kama NGO na linapata mabilioni ya fedha na huko watu wanatetea ulaji kwa mgongo wa waandishi, wanahabari watajitungia kanuni wenyewe , code of ethics zao na hata Bodi wajumbe wake saba, wanne wanahabari watatokana na wenyewe,” alifafanua.
Kuhusu ushiriki wa wadau wa habari kwenye muswada huo, Nape alisema si kweli kwamba hawajashirikishwa kama inavyodaiwa na baadhi ya wabunge wa upinzani, bali walishiriki kwenye hatua ya kabla muswada kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri, wakati ukiandaliwa na baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni na kupelekwa kwenye kamati.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupitishwa muswada huo, Nape amewaomba wadau wa habari kuisaidia serikali kwenye utungaji wa kanuni za sheria hiyo pamoja na kuwataka wanahabari walioonesha kujigawa kutokana na muswada huo, kuungana tena kuijenga tasnia ya habari.
“Serikali ipo tayari kuwashirikisha wadau wa habari kwenye utungaji wa kanuni na tunaamini haitachukua muda mrefu kukamilishwa kwa kanuni hizo na pia ifahamike utekelezaji wa sheria hiyo utahitaji ushirikiano,” alisema.
Nape pamoja na kuwashukuru wadau wa habari, walioshiriki kusaidia kufanikisha safari ya miaka 23 ya utungwaji wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 na kufanya kazi hiyo kuwa nyepesi kwa upande wa serikali.
“Mchakato ulionesha dalili ya kugawa tasnia, tutafute namna ya kuirudisha tasnia pamoja. Tuzike tofauti zetu, tukae pamoja tujenge tasnia... nawaomba tusahau tofauti zetu,” alisema.
0 Maoni:
Post a Comment