Mkuu wa Wilaya Ya Kinondoni, Ally Hapi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni kumvua madaraka mratibu wa TASAF wa wilaya hiyo, Onesmo Kweyamba kutokana na kasoro mbalimbali zilizosababisha upotevu wa fedha za serikali kwa kuwapatia kaya ambazo hazikustahili kupewa kupitia mradi wa TASAF.
Akizungumza na waandishi wa habari, Hapi amesema fedha taslimu kiasi cha 180,323,000/= zililipwa kwa kaya 515 ambazo hazikuwa na sifa za kulipwa kulingana na sifa zilizoainishwa huku wananchi wenye sifa wakiachwa.
Aidha, wawakilishi 537 wa kaya wamelipwa kiasi cha shilingi 266,008,000/= huku wahusika waliokuwa wakipokea pesa hizo kushindwa kujulikana makazi yao yalipo baada ya uhakiki kufanyika.
Ulipaji wa watu hao umeelezwa kusimamishwa hadi uhakiki mwingine utakapofanyika kwa kushirikisha vyombo vya dola na kubainisha zilipo kaya hizo ili kujua kama zina sifa za kupewa fedha hizo au la.
Baadhi ya waliokuwa wakilipwa fedha hizo za kaya masikini ni pamoja na baadhi ya watumishi wa serikali, sekta binafsi na watu wenye biashara mbalimbali zinazowaingizia kipato kinyume na masharti ya TASAF.
Hapi amesema, jumla ya kaya 1397 zimebainika kuwa na upungufu wa sifa za kupatiwa fedha hizo za mradi wa TASAF katika wilaya ya Kinondoni na hivyo kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Mkuu huyo wa wilaya ameagiza vyombo vya dola wilayani Kinondoni kuanza uchunguzi mara moja dhidi ya wale wote walioshiriki kuhujumu fedha za serikali na kufanya udanganyifu huo kwa awamu saba tofauti za malipo yaliyofanyika tangu July, 2015.
0 Maoni:
Post a Comment