MKAZI wa Nyegezi jijini Mwanza, Soli Mkanzabe (24), anashikiliwa na
Polisi akituhumiwa kumbaka na kumjeruhi sehemu za siri mtoto wa miaka
minne (jina limehifadhiwa).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema jijini humo
kuwa, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la jinai Februari 26, mwaka huu,
saa 10 jioni katika mtaa wa Password.
"Inadaiwa mtuhumiwa alifika nyumbani kwao mtoto huyo na kumkuta
akicheza na wenzake akamwita waende chumbani kwake," amesema Kamanda
Msangi na kuendelea:
"Mtoto alimfuata kwenda chumbani na baadaye mtuhumiwa alimfanyia
ukatili wa kumbaka na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri, huku
akimuonya asiseme kwa mtu yeyote jambo hilo."
Amesema, baada ya mtoto huyo kufanyiwa ukatili huo, hakumwambia mtu,
lakini mama yake aliporudi kutoka kazini alimuogesha na kugundua
amebakwa, ndipo alitoa taarifa kituo cha Polisi.
"Polisi walifanya ufuatiliaji haraka eneo la tukio na kufanikiwa
kumkamata mtuhumiwa.
Wanaendelea kupeleleza na kumhoji mtuhumiwa.
Uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yake," amesema Msangi.
Mtoto huyo alipatiwa matibabu Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana na hali yake inaendelea vizuri.
0 Maoni:
Post a Comment