RAIS John Magufuli amewapongeza madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Neema Wambura ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.
Pongezi hizo za Dk Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa maendeleo ya afya yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, katika pongezi hizo, Dk Magufuli alisema madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na ambayo yalitishia uhai wake.
Pia alimpongeza Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa upendo wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake huko Tandika Davis Kona jijini Dar es Salaam.
“Nakushukuru sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya,” Ikulu imekariri Rais Magufuli akisema.
Kabla ya kutoa pongezi hizo, jana asubuhi, Rais Magufuli aliwatuma wasaidizi wake wakiongozwa na Msigwa kwenda Tandika Davis Kona katika Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, kumuona Neema ambaye alipatiwa hifadhi katika nyumba ya mama mjane, Mariam Amir (Bibi Mwanja) baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika mitandao ya kijamii.
Rais Magufuli ametoa Sh 500,000 kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia chakula yeye na watoto wake, waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda mkoani Mara na pia alitoa Sh 500,000 kwa Bibi Mwanja aliyejitolea kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake. Pia ameahidi kumsaidia wakati wote wa matibabu na pia familia yake.
Baada ya kumpokea, Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura na ajali katika Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga alisema wameanza kumfanyia uchunguzi ili kujua maendeleo yake na kama kumpa matibabu zaidi.
Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk Ibrahim Mkoma ambaye amekuwa akimfanyia matibabu Neema tangu Julai 2015 alipofikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza, alisema mwanamke huyo anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji mara nne.
Dk Mkoma alisema baada ya upasuaji huo, sasa anaweza kuinua na kugeuza shingo yake na kwamba kwa sasa wataendelea kumfanyia uchunguzi zaidi ili kujua maendeleo yake. Rais Magufuli ameagiza vyombo vyote vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema na kuhakikisha haki inatendeka.
0 Maoni:
Post a Comment