MATUKIO ya mauaji na kujeruhi viongozi na wananchi katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, yameendelea kuripotiwa, ikielezwa katika usiku wa kuamkia jana, watu watatu akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji kwenye Kijiji cha Nyamisati wilayani Kibiti, wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika.
Hata hivyo, taarifa za baadaye kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga zilieleza kuwa watu wasiojulikana wamejeruhi na kuteka watu watatu na kusisitiza kuwa, hana taarifa za kutokea kwa vifo.
Alisema hawezi kuthibitisha kwa kuwa hajapata taarifa za kuuawa kwa watu, zaidi ya kuambiwa wametekwa na kupelekwa kusikojulikana. “Tunaendelea kufuatilia tukio hilo kujua kama ni kweli wameuawa au la na hadi sasa haijulikani watu gani waliowateka watu hao ila uchunguzi bado unaendelea kufanyika kujua ukweli wa tukio hilo,” alisema Lyanga.
Awali, ilielezwa wanaodaiwa kuuawa kuwa ni Moshi Machela ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji, Hamid Kidevu na Yahaya Makame. Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamhussein Kifu alisema tayari amemtuma Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kufuatilia tukio hilo ili kuweza kuthibitisha kama tukio hilo lipo. Kifu alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa kamili watazitoa juu ya tukio hilo.
0 Maoni:
Post a Comment